1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP25: Joto kali kuathiri zaidi afya ya binaadamu

3 Desemba 2019

Mkutano wa kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi unaendelea katika mji mkuu wa Uhispania Madrid. Katika kikao cha leo wajumbe wamezungumzia jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyoaathiri afya ya binadamu.

https://p.dw.com/p/3UA6G
A worker walks past a COP 25 logo at IFEMA Convention Center, ahead of the 2019 U.N. climate change conference (COP 25) in Madrid
Picha: REUTERS

Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri afya ya binaadam kutokana na ile hali kwamba watu wengi wanasumbuliwa na kishindo cha joto, hali ya hewa iliyokithiri na maradhi yanayosababishwa na mbu ikiwa ni pamoja na malaria, limesema hayo shirika la afya la kimataifa WHO.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema katika ripoti yake iliyochapishwa hii leo katika mkutano wa mabadiliko ya tabianchi mjini Madrid limewahimiza viongozi wa serikali wayafikie malengo yaliyowekwa ya kupunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani, moshi  unaosemekana kuwa sababu ya kuzidi hali ya ujoto ulimwenguni.

Shirika hilo la afya la kimataifa linasema katika ripoti yake kwa namna hiyo maisha ya watu milioni moja yataweza kunusurika kwa mwaka ikiwa viwango vinavyochafua hewa havitakuwa vya juu sana.

Shirika la WHO linakadiria kwamba mabadiliko ya tabianchi ndio kitisho kikubwa kwa afya katika karne ya 21. "Sababu ya hali hiyo ni moja tu kama hatutopunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani, tutaendelea kuharibu ugavi wa chakula, ugavi wa maji na hewa safi na vitu vyote ambavyo tunavihitaji ili tuweze kuwa na afya nzuri" amesema mtaalam wa shirika la afya la kimataifa Diarmid Campbell-Lendrum.

UN-Klimakonferenz 2019 | Cop25 in Madrid | Greta Thunberg, schwedische Klimaaktivistin
Greta Thunberg, mwanaharakati kijana wa utetezi wa mazingira alipowasili bandari ya Santo Amaro, mjini Lisbon.Picha: Reuters/P. Nunes

Nalo shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia masuala ya hali ya hewa linautaja muongo huu tulionao kuwa ndio utakaoweka rekodi mpya ya hali ya ujoto ulimwenguni. Shirika hilo la hali ya hewa linasema data za awali zinaonyesha kipindi cha mwaka 2015 hadi mwaka 2019 na kutoka mwaka 2010 hadi 2019 ni vipindi ambavyo hali ya joto ilikithiri kupita kiasi.

Katika ripoti yake iliyochapishwa pia mjini Madrid hii leo kwenye mkutano unaojadili mabadiliko ya tabianchi, COP25 shirika hilo linasema mkondo huo utaendelea na kugeuka kuwa mwongo ambao joto lilikuwa kali kupita wakati wowote ule tangu mwaka 1980.

Wakati huo huo mwanaharakati kijana mpigania utunzaji wa mazingira Greta Thunberg amewasili Lisbon leo baada ya kuizunguka bahari ya Atlantiki kwa mashua ambapo atashiriki katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi mjini Madrid.

Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi ulioanza jana utamalizika Disemba 13. Wawakilishi wa mataifa 200 yaliyotia saini mkataba wa mabadiliko ya tabianchi wa Paris mnamo mwaka 2015 wanahudhuria mkutano huo wa Madrid.