Colombia yasitisha mashambulizi dhidi ya FARC
11 Machi 2015Tangazo hilo lililotolewa jana (10 Machi) na Rais Juan Manuel Santos linafuatia lile la miezi mitatu nyuma, ambapo wapiganaji hao wa msituni walisema wangelisitisha mashambulizi yoyote dhidi ya majeshi ya serikali kuanzia tarehe 20 Disemba, ingawa walionya kuwa msimamo huo ungeliondoshwa endapo wangelishambuliwa.
Na sasa, baada ya kukataa wito wa kuwa na makubaliano ya pande mbili ya kusitisha mapigano, Santos amesema serikali yake itasitisha mashambulizi kwa kipindi maalum, hatua ambayo baadaye itatathminiwa upya.
"Kwa ajili ya kuukwamua mzozo huu, nimeamua kuiamuru wizara ya ulinzi na makamanda wa jeshi kuacha kuzishambulia kwa mabomu kambi za FARC kwa kipindi cha mwezi mmoja. Baada ya hapo, tutathmini utekelezaji wa usitishaji mapigano wa upande mmoja na kwa mujibu wa matokeo hayo ndipo tutaamua ikiwa tuendelee na hatua hii ama la," alisema Rais Santos.
Mashambulizi dhidi ya ELN kuendelea
Hata hivyo, tangazo hili la Rais Santos halimaanishi kusitishwa kwa mashambulizi dhidi ya makundi mengine ya waasi, kama lile la ELN, lenye wapiganaji wapatao 1,500 na ambalo ni la pili kwa ukubwa baada ya FARC, ingawa nalo limo kwenye mazungumzo yasiyo rasmi na serikali.
Wajumbe wa serikali na wa kundi la FARC wanaokutana mjini Havana, Cuba, wamefikia sehemu fulani ya makubaliano juu ya mageuzi katika sera ya ardhi, ushiriki wa kisiasa wa wapiganaji wa zamani wa msituni, na kukomeshwa kwa biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Hata hivyo, masuala muhimu ya kuvunjwa kwa kundi hilo la waasi na kufidiwa kwa wahanga wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe bado yanajadiliwa, huku Rais Santos akitangaza kuungwa kwa Kamisheni ya Amani kusaidia duru ya mwisho ya mazungumzo.
“Nimeamua kuunda Kamati ya Ushauri kwa ajili ya amani ambayo itawajumuisha wote na ambayo itakusanya maoni ya wananchi mbalimbali. Litakuwa kundi la raia mashuhuri wa Colombia wenye uzoefu, uhuru na dhamira yao kwa nchi haina shaka. Kamati hii itanishauri na kuwa nami kwenye mchakato wa hatua ya mwisho ya kupatikana kwa amani,“ alisema Santos.
Raia wa Colombia watapiga kura ya maoni kabla ya makubaliano ya mwisho kutekelezwa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo