1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yashtumiwa kuwapangisha uzazi kwa lazima Waiughur

29 Juni 2020

Maafisa wa serikali China wameshutumiwa kuwalazimisha wanawake wa jamii ya Uighur kupanga uzazi, ikiwa ni kampeni inayolenga kupunguza ukuaji wa idadi ya Waighur, kulingana na ripoti ya utafiti iliyochapishwa Jumatatu.

https://p.dw.com/p/3eWIC
München Uiguren Protest gegen China
Picha: picture-alliance/Zuma/S. Babbar

Ripoti hiyo ambayo imejikita kwenye mkusanyiko wa data rasmi za serikali, stakabadhi za sera pamoja na mahojiano na wanawake wa jamii ndogo ikiwemo ya Waighur, imelifanya kundi la wabunge kuutakaUmoja wa Mataifa kuzichunguza sera za China katika jimbo hilo.

Huenda hatua hiyo itaighadhabisha China ambayo imekuwa ikikanusha madai ya kukiuka haki za makabila katika jimbo la Xinjiang. Tayari China imeyataja madai kwenye ripoti ya Jumatatu kuwa "yasokuwa na msingi."

Nchi ya China imeshutumiwa kwa kuwafungia zaidi ya Waighur milioni moja pamoja na jamii nyingine ndogo za Waislamu kwenye kambi za kuwapa elimu. China inazitaja kambi hizo kuwa vituo vya kutoa mafunzo ya kazi yanayolenga kuwaepusha watu kujihusisha na mambo ya kigaidi, kufuatia misururu ya machafuko yanayodaiwa kufanywa na makundi yanayotaka kujitenga.

Ripoti hiyo ya mtafiti wa Ujerumani Adrian Zenz, ambayo imefichua sera za China katika jimbo la Xinjiang, inasema kuwa wanawake wa jamii ya Uighur wanatishiwa kufungwa katika kambi kwa kukataa kuavya mimba ikiwa wamepitiliza idadi ya watoto iliyokubaliwa.

Symbolbild UN-Experten werfen China Missachtung Menschenrechte vor
Maandamano dhidi ya madai ya mauaji ya Waighur na serikali ya ChinaPicha: Getty Images/AFP/T. A. Clary

Jopo la wataalam wa UN pia laishutumu China

Awali, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaochunguza matukio ndani ya kambi hizo, wamewahi kunukuu ripoti ya utafiti wa Zenz ambao umehusisha nyaraka za umma katika tovuti ya China.

Ripoti imeeleza kuwa wanawake waliokuwa wamezaa watoto wachache kulingana na wanaokubaliwa kisheria, waliwekewa vifaa vya kupanga uzazi IUD. Imeongeza pia kwamba baadhi ya wanawake walisema walikuwa wakishawishiwa kukubali kufanyiwa upasuaji wa kuwahasi.

Wanawake waliofungwa zamani katika kambi hizo wamedai kwamba walidungwa sindano ya kusitisha hedhi au iliyosababisha uvujaji damu usio wa kawaida kutokana na athari za dawa za kupanga uzazi.

Nyaraka za serikali ambazo Zenz amechambua, zimeonyesha kuwa baadhi ya wanawake wa jamii ndogo katika vijiji vya jimbo hilo walifanyiwa uchunguzi wa lazima mara kwa mara kuhusu afya ya uzazi pamoja na uchunguzi wa ujauzito mara mbili kila mwezi.

Mpango wa China umesababisha idadi ya jamii kushuka?

Zenz alibaini kwamba ukuaji wa idadi ya watu katika majimbo ya Xinjiang, ambayo ni nyumbani kwa jamii ndogo, ulishuka chini ya wastani, haswa kwa kabila la Han kati ya mwaka 2017 na 2018, mwaka mmoja baada ya rekodi rasmi za watu kuhasiwa katika eneo hilo kushinda viwango vya uhasi wa mwaka 2016.

Wanaharakati wa jamii ya Uighur wamesema China inatumia kambi za kuwafunga watu kuendeleza kampeni pana ya upotoshaji kwa lengo la kutokomeza utamaduni wao na utambulisho wao wa Uislamu.

Zenz ameandika kwenye ripoti kwamba, China inaonekana kuendeleza mpango wa uzazi kwa njia ya ushawishi, kama mpango mpana wa kiubaguzi kudumaza ukuaji wa makabila mengine.

Berlin Uiguren Protest
Maandamano mjini Berlin dhidi ya wanayopitia WauighurPicha: Getty Images/S. Gallup

"Haya yaliyobainika yanaibua wasiwasi mwingi ikiwa sera za China katika Xinjiang zinawakilisha kwa njia ya msingi, kile kinachoweza kutizamwa kama kampeni ya mauaji ya kimbari, kwa mujibu wa ufafanuzi wa Umoja wa Mataifa." Ripoti imesema.

IPAC yataka uchunguzi wa kisheria dhidi ya China

Muungano wa wabunge kuhusu China wanaotoka katika vyama mbalimbali vya kisiasa nchi za Amerika ya Kusini, Ulaya na Australia (IPAC), umesema Jumatatu kwenye taarifa kwamba utashinikiza uchunguzi wa kisheria ufanywe kubaini ikiwa mambo hayo si sawa na uhalifu dhidi ya ubinadamu au hata mauaji ya kimbari eneo la Xinjiang.

Kundi la wanaharakati World Uighur Congress limesema ripoti imeonyesha kipengele cha mauaji ya kimbari ya sera za chama cha Kikomunisti cha China (CCP) na limetoa mwito wa hatua za kimataifa kuchukuliwa kuikabili China.

Lakini wizara ya Mambo ya nchi za nje wa China imesema madai hayo hayana msingi na yanaonyesha dhamira fiche.