1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muumano wa biashara kati ya Marekani na China watokota

Shisia Wasilwa
11 Julai 2018

China imeishtumu Marekani kwa vitisho na kuonya kuwa itajibu, kufuatia hatua ya utawala wa rais Donald Trump kuzidisha mzozo wa kibiashara kwa kutishia kuweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa za China.

https://p.dw.com/p/31GLn
Symbolbild zur drohenden Zuspitzung des Handelskrieg s zwischen den Vereinigten Staaten von Amerika
Picha: imago/R. Peters

Bidhaa hizo za China ni za thamani ya dola bilioni 200. Wizara ya biashara ya China imeeleza kushtusha na kusema itapeleka malalamiko kwa shirika la biashara duniani WTO, lakini haikuonyesha mara moja namna itakavyojibu. 

Taarifa ya wizara ya Biashara ya China ilisema kuwa, hatua ya Marekani ya kuchapisha orodha ya bidhaa zitakazotozwa ushuru haikubaliki kamwe. Iliendelea kusema kuwa serikali ya China italazimika kuchukua hatua madhubuti kuyalinda maslahi yake.

Taarifa hizo zimesababisha kushuka kwa hisa za masoko, huku masoko ya China yakiongoza kwenye mdororo huo, hatua ambayo imelazimisha afisa mkuu wa biashara katika wizara ya Biashara nchini humo kuonya kuwa Marekani itavuruga biashara ya Ulimwengu.

Marekani yachapisha orodha ya bidhaa 

Maafisa wa Marekani walichapisha orodha ya maelfu ya bidhaa za China ambazo zitatozwa ushuru mpya zikiwemo vyakula, tumbako, kemikali, makaa ya mawe, chuma cha pua na bati.

Bidhaa hizo pia zinajumuisha matairi, samani, vipochi vya kina mama, vyakula vya paka na mbwa, mazulia, milango, na bidhaa za urembo.

Rais wa Marekani Donald Trump kulia na Rais Xi Jinping wa China kwenye mkutano wa biashara 2017
Rais wa Marekani Donald Trump kulia na Rais Xi Jinping wa China kwenye mkutano wa biashara 2017Picha: Getty Images/AFP/N. Asfouri

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, utawala wa Trump umekuwa ukihimiza China kusitisha biashara zake zinazokandamiza Marekani na badala yake kufungua soko lake na kushiriki kwenye biashara yenye ushindani, alisema mwakilishi wa Biashara wa Marekani Robert Lighthizer, alipokuwa akitangaza mapenedekezo ya ushuru huo mpya.

Aliongeza kusema kwenye taarifa kuwa, badala ya kuelezea wasiwasi wa Marekani, China imeanza kulipiza kisasi dhidi ya bidhaa za Marekani, na kusisitiza kuwa hawana haki kwenye hatua yao waliochukua.

Juma lililopita Washington iliweka ushuru wa asilimia 25 kwa bidhaa za China zenye thamani ya dola bilioni $34. Beijing ilijibu mara moja kwa kuziwekea ushuru sawa bidhaa ambazo Marekani inauzia China.

Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: picture-alliance/abaca/O. Douliery

Hofu ya wawekezaji 

Wawekezaji wanahofu kuwa kuongezeka kwa mzozo wa biashara kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani huenda, kukaathiri ukuaji wa uchumi ulimwenguni.

Rais Donald Trump amesema, mwishowe huenda akaongeza ushuru kwa bidhaa za China zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 500, karibu jumla ya bidhaa zote ambazo Marekani iliziagiza kutoka China mwaka jana.

Ushuru huo hautatekelezwa hadi kipindi cha miezi miwili ambapo umma utapewa nafasi ya kutoa maoni kuhusu orodha ya bidhaa zilizopendekezwa kutozwa ushuru, lakini baadhi ya makundi ya wafanyibiashara na wajumbe walikosoa haraka hatua hiyo.

Chama cha wafanyabiashara wa Marekani kimesema kuwa: "Rais amekiuka ahadi ya kuiumiza China kwa kiwango kikubwa na badala yake wateja ndio wanaothirika."

Waziri mdogo wa biashara wa China Li Chenggang, amesema kuwa China haina budi kupambana na Marekani. Ameongeza kuwa lazima waweke mikakati kabambe ili kupunguza gharama kwa wateja wake na kufungua uchumi wake kwa wawekezaji wa kimataifa.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Reuters, Ap

Mhariri:Iddi Ssessanga