1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Korea Kaskazini kuimarisha uhusiano

21 Juni 2019

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais wa China Xi Jinping wamekubaliana kuimarisha mahusiano yao katika kipindi ambacho mataifa hayo yapo kwenye wakati mgumu wa kimahusiano ya kimataifa.

https://p.dw.com/p/3KpGk
Xi Jinping in Nordkorea mit Kim Jong Un
Picha: Reuters/KCNA

Xi ameondoka katika viunga vya mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang mapema leo baada ya kuwepo nchini humo kwa siku mbili, ikiwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa China kufanywa katika kipindi cha miaka 14. Kiongozi huyo alipokewa kwa shangwe na idadi kubwa ya wananchi waliobeba mabango yenye picha yake, bendera ya China sambamba na nyimbo zenye kuhamasisha upendo kwa china.

China ni mshirika pekee mkubwa wa Korea Kaskazini na ziara ya Xi Jinping ilikuwa na lengo la kuliimarisha taifa hilo lilolotengwa kutokana na vikwazo vya Umoja wa Mataifa, vilivyotokana na matumizi yake ya nyuklia na mpango wake wa makombora, jambo ambalo pia limetiwa chumvi na kuvunjika kwa mazungumzo ya kuachana na matumizi ya nishati hiyo na Marekani.

Pongezi za jitihada za kuachana na matumizi ya nyuklia

Xi Jinping in Nordkorea mit Kim Jong Un
Mkutano wa rais Xi Jinping na kiongozi wa Korea Kim Jong UnPicha: Reuters/KCNA

Kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kaskazini KCNA Rais Xi amezipongeza jitihada za Korea Kaskazini katika kuachana na matumizi ya nyuklia na kuongeza kuwa dunia ina matumaini kwamba taifa hilo na Marekani watafanya mazungumzo yatakayozaa matunda.

Aidha wamekubaliana kuendeleza kile walichosema mawasiliano ya kimkakati na kufanikisha umadhubiti wa ushirikiano katika nyanja zote. Ingawa wajuzi katika masuala ya haki za binadamu wanasema zipo ishara kwamba China imekuwa na ushirikiano na Korea Kaskazini, katika kufanikisha ukamatwaji wa raia wa Korea Kaskazini waliolitoroka taifa hilo.

Baadhi ya raia wa Korea waikosoa ziara ya Xi Jinping

Baadhi ya raia wa Korea Kaskazini walikuwa na maoni tofauti baada ya hitimisho la ziara hiyo ya siku mbili. Lee Kyu-min mwenye umri wa miaka 26 ni mwanafunzi. "Baada ya viongozi wawili wa Korea kukutana tulikuwa katika uelekeo wa kuboresha uhusiano wetu. Nafikiri mkutano kati ya Korea na China utaikwamisha hatua hiyo."

Kijana mwingine askari wa taifa hilo, Moon Ji-won mwenye umri wa miaka 25 alitoa mtazamao wake."Nafikiri mkutano huo ni mbaya sawa kwa taifa letu. Sina mashaka na uhusiano wetu na Marekani, kwa kuwa tumekuwa na ushirikiano mzuri, lakini ukweli China na Korea Kaskazini wanafanya mkutano wenye matokeo mabaya dhidi yetu."

Ziara ya Xi Jinping imefanyika katika kipindi kisichozidi wiki moja kabla kiongozi huyo na Rais Donald Trump kukutana katika mkutano wa matiafa 20 yalipiga hatua kubwa kiviwanda duniani yaani G20, ambao safari hii utafanyika nchini Japan. Mkutano huo unagubikwa na mgogoro wa kibiashara ambao umelivuruga soko la fedha la dunia.

Mwandishi: Sudi Mnette RTR
Mhariri: Sekione Kitojo