1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za usajili wa wapigakura nchini Kongo

Jean Noël Ba-Mweze
9 Februari 2023

Ni watu wapatao milioni 12 pekee waliojisajili kama wapigakura magharibi mwa Kongo . Tume ya uchaguzi inatarajia kusajili wapigakura milioni 50 kote nchini.

https://p.dw.com/p/4NGwn
Tume ya uchaguzi yatangaza idadi ya mwanzo ya wapigakura waliojisajili kwenye majimbo ya magharibi mwa Kongo
Tume ya uchaguzi yatangaza idadi ya mwanzo ya wapigakura waliojisajili kwenye majimbo ya magharibi mwa KongoPicha: Getty Images/AFP/J. Wessels

Tume huru ya uchaguzi, CENI,ilikuwa imepanga kusajili wapiga kura milioni 18 kwenye Daftari la Wapigakura katika eneo la kwanza la operesheni hiyo, yaani magharibi mwa nchi hii ambayo inajumuisha mikoa kumi ukiwemo pia Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Chini ya siku kumi kabla ya kumalizika usajili ambao mwisho wake umepangwa Februari 17, CENI inawaomba Wakongo wote ambao wana haki ya kujiandikisha, kuharikisha muda huu wa siku chache zinazobaki ili kupata kadi zao za wapiga kura.

Wapigakura milioni 50 wamekadiriwa kusajiliwa

Matokeo hayo, ambayo bado ni ya muda yametolewa na Patricia Nseya, msemaji wa CENI.

"Kazi za uchunguzi za CENI katika eneo la kwanza la usajili zinaonyesha kwamba idadi ya wapiga kura inayotarajiwa ni zaidi ya milioni 18 na hadi sasa, zaidi ya milioni 12 tayari wamejiandikisha, yaani asilimia 64.35. Kwa hiyo, safari ya  uchaguzi huru, wa kidemokrasia na wa wazi ndani ya muda wa kikatiba haiwezi kurudi nyuma."

Lakini bado sio rahisi Wakongo kufanikiwa kuandikishwa na hivyo kupata kadi kutokana na sababu nyingi zikiwemo upungufu wa vifaa vya uandikishaji, huku idadi ya watu ikiwa kubwa, kuharibika mara kwa mara kwa vifaa hivyo pamoja na baadhi ya wananchi kulazimishwa kutoa rushwa ili kuandikishwa.

''Mimi tayari nimepata ila kwa shida''

Wakongo zaidi ya milioni 12 tayari wamepata kadi zao za kupigakura eneo la magharibi mwa Kongo
Wakongo zaidi ya milioni 12 tayari wamepata kadi zao za kupigakura eneo la magharibi mwa KongoPicha: Getty Images/AFP/C. Thirion

Mmoja wao ni François Tshitenga, mkaazi wa wilaya ya Bel Air mashariki mwa Kinshasa, ambaye alifanikiwa kupata kadi yake katika shule la Sikama ambacho ni kituo cha usajili kilichopo katika wilaya ya Badara ya tatu katika eneo la N'Sele baada ya kujaribu mara tano.

"Hii ni kwa ujumla ila imethibitishwa sana katika mtaa wetu. Matatizo ni mengi sana hapa kwetu na hivyo wakaazi wengi huenda kujiandikisha mahali pengine kwani hapa vifaa huharibika kila mara. Ni lini watu hawa wote wanaosubiri hapa watapata kadi zao? Mimi tayari nimepata ila kwa shida. Hatimaye nina furaha ila wasiwasi wangu ni watu hawa walio hapa nje wakipigwa na jua."

Mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haijawapa raia wa Kongo kitambulisho kwa zaidi ya miaka 25. Na hivyo ni kadi ya mpiga kura ndiyo hutumika kama kitambulisho nchini humu.