1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Chama kikuu cha upinzani chavunjwa Senegal

Saleh Mwanamilongo
1 Agosti 2023

Watu wawili waliuawa Jumatatu wakati wa maandamano nchini Senegal baada ya kufunguliwa mashtaka na kuzuiliwa kwa kiongozi wa upinzani, Ousmane Sonko.

https://p.dw.com/p/4UdNB
Watu wawili wafariki dunia kufuatia maandamano Senegal
Watu wawili wafariki dunia kufuatia maandamano SenegalPicha: NGOUDA DIONE/REUTERS

Wizara ya mambo ya ndani ya Senegal imesema maandamano yalizuka Jumatatu alasiri katika mji wa kusini wa Ziguinchor ambapo watu wawili waliuliwa. Hata hivyo taarifa hiyo haikutoa ufafanuzi kuhusu mazingira ya vifo vya waandamanaji hao wawili katika jiji ambalo Ousmane Sonko ni meya.

Sonko, mkosoaji mkali wa Rais Macky Sall, Jumatatu alishtakiwa kwa kuchochea uasi, hali ambayo ilisababisha maandamano na purukushani baina ya polisi na waadamanaji.

Masaa mawili tu baada ya Sonko kufunguliwa mashtaka, wizara ya mambo ya ndani ilitangaza kuwa chama chake cha kisiasa cha PASTEF kimevunjwa kufuatia agizo la rais.

Waziri wa mamabo ya ndani Antoine Abdoulaye Diome katika taarifa kwa vyombo vya habari, alihalalisha uamuzi wake kwa kile alichosema ni mito ya mara kwa mara kwa harakati za uasi iliotolewa na chama hicho cha upinzani, na  ambazo kulingana na waziri huyo zilisababisha vifo vingi mnamo mwezi Machi 2021 na mwezi Juni 2023.

Mamlaka nchini Senegal zimesema chama cha upinzani cha PASTEF kimehusika pia na ukiukaji wa kudumu na mkubwa wa majukumu ya vyama vya siasa.

PASTEF yakashifu hatua ya serikali

Ousmane Sonko, kinara wa upinzani  na meya wa jiji la Ziguinchor kusini mwa Senegal
Ousmane Sonko, kinara wa upinzani na meya wa jiji la Ziguinchor kusini mwa SenegalPicha: Seyllou/AFP

Chama hicho cha upinzani kilikashifu hatua hiyo, kikisema katika taarifa yake kwamba uthabiti wa nchi hiyo sasa umetatizwa, na kwamba hatua ya kuvunjwa kwa chama hicho ni kupinga demokrasia.

Serekali ya Senegal jana ilitangaza pia kusitisha huduma zote za mtandao wa Intanteti kwa kile imesema ni kutokana na kusambaa kwa "ujumbe wa chuki" kupitia mitandao ya kijamii.

Wakili wa Sonko, Babacar Ndiaye amesema bugdha zote za serikali ni njama ya kumzuia Sonko kuwania urais.

"Tunafikiri ilikuwa ni amri ya kisiasa ambayo kwa bahati mbaya ilitekelezwa na jaji. Lengo la agizo hili la kisiasa lilikuwa kumzuia Rais Ousmane Sonko kushiriki uchaguzi wa 2024. Na kwa bahati mbaya, leo tuna mahakama ambayo ni tiifu kwa serikali. Na hiyo ni ishara mbaya kwa demokrasia yetu ya Senegal.", alisema Ndiaye.

Mapema hapo jana, mgombea huyo wa urais katika uchaguzi wa mwaka 2024, Ousmane Sonko, alishtakiwa na jaji ambaye aliamuru azuiliwe hasa kwa "wito wa uasi na njama" dhidi ya Serikali.

Kesi za kisiasa dhidi ya Sonko ?

Ousmane Sonko ni mkosoaji mkubwa wa rais Macky Sall
Ousmane Sonko ni mkosoaji mkubwa wa rais Macky SallPicha: Presidency of Senegal / Handout/AA/picture alliance | Seyllou/AFP/Getty Images

Siku ya Ijumaa, Ousmane Sonko alikamatwa nyumbani kwake. Aliporudi kutoka kwenye swala ya Ijumaa, rais wa PASTEF alidai kuwa alimpokonya simu polisi aliyekuwa akimrekodi bila idhini yake. Kitendo ambacho mamlaka nchini Senegal imekiita kuwa wizi wa kutumia nguvu.

Ousmane Sonko, mwenye umri wa miaka 49, hivi sasa anakabiliwa na kesi nyingine ya tatu, ambayo inaweza kuhatarisha zaidi ushiriki wake katika uchaguzi wa urais wa Februari mwakani.

Sonko, tayari alihukumiwa Juni Mosi hadi miaka miwili jela kwa rushwa kwa vijana. Uamuzi huo wa mahakama ulisababisha ghasia na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 15.

Chanzo : AFP