1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CCM yatangaza mchakato wa kupata wagombea

12 Juni 2020

Chama tawala Tanzania CCM, kimetangaza ratiba ya mchakato wa kupata wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, huku kikisisitiza maadili na maono ya wagombea ni miongoni mwa sifa zitazozingatiwa.

https://p.dw.com/p/3dhPD
Tansania CCM-Generalsekretär Amtsübergabe Abdurahman Kinana & Bashiru Ally
Picha: DW/E. Boniface

Kwa mujibu wa ratiba iliotolewa na katibu mwenezi wa chama hicho Humphrey Polepole, mchakato wa uchukuaji fomu, utaanza June 15 ambapo watia nia watatumia siku 15 hadi kurejesha fomu itakayo dhaminiwa na wananchama zaidi ya 200 kwa upande wa Urais Zanzibar na wananchama wasiopungua mikoa 15 kwa upande wa Jamhuri.

Kukamilika kwa zoezi la urejeshaji wa fomu kutatoa fursa kwa kikao cha Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kitakachoanzisha mchakato wa uchujaji majina kisha tarehe 8 Julai 2020 kitaketi kikaocha Kamati ya Usalama na Madili ya chama hicho.

Mapendekezo kutolewa Julai 9

Polepole amewaambia wanahabari kuwa Julai 9, Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chake kitatoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano, wanaoomba kugombe anafasi hiyo.

Akitaja sifa za wagombea mbali na kutilia mkazo maadili kwa kada wataowania katika nafasi hizo nyeti, Polepole amesema kinahitaji wagombea ambao watakuwa na mtazamo unaofanana na Rais na si wavurugaji.

Katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba CCM Zanzibar inataraji kupata Sura mpya katika nafasi ya urais baada ya Rais wa sasa dokta Mohammed Shein kumaliza awamu zake mbili za uongozi.

Mwezi Oktoba Tanzania inataraji kufanya uchaguzi utaowaweka mamlakani madiwani, wabunge na Rais ambapo Rais John Magufuli anatarajiwa kutetea kiti hicho kwa awamu ya pili ya uongozi na ya mwisho kwa mujibu wa katiba ya taifa hilo la Afrika mashariki.