Burkina Faso yajiandaa kwa maandamano mapya
2 Novemba 2014Hali hiyo inaiweka Burkina Faso katika hali ya kutokea maandamano mapya nchini humo.
Uongozi wa juu wa jeshi umemtaja Luteni kanali Issac Zida, naibu kamanda wa kikosi cha ulinzi wa rais, kuwa mkuu wa nchi jana Jumamosi. Mvutano wa kuwania madaraka ndani ya majeshi ya ulinzi ulitatuliwa baada ya mkuu wa jeshi hilo kuwekwa kando.
Ajitangaza rais wa mpito
Zida, ambaye ana udhibiti katika utendaji wa kikosi hicho kilichopata mafunzo ya hali ya juu na vifaa bora, alijitangaza kuwa rais wa mpito mapema jana kupitia hotuba aliyoitoa redioni, akifuta madai ya mkuu wa majeshi Honore Traore ya kuliongoza taifa hilo katika kipindi cha mpito kufuatia kuondoka madarakani kwa rais Compaore.
Mmoja kati ya marais wa Afrika aliyetawala kwa muda mrefu , Compaore alijiuzulu siku ya Ijumaa baada ya siku mbili za maandamano ya umma dhidi ya juhudi zake za kubadilisha katiba kurefusha muda wake wa miaka 27 madarakani. Kiasi watu watatu wameuwawa baada ya waandamanaji kuvamia jengo la bunge na kulichoma moto jengo hilo.
Katika mitaa yenye vumbi ya mji wa Ouagadougou , mji mkuu wa Burkina Faso, waandamanaji wameelezea hasira zao kwamba na kwamba wamemuondoa madarakani Compaore, ambaye alikamata madaraka mwaka 1987 katika mapinduzi ya kijeshi - na sasa yuko mwanajeshi mwingine ambaye anataka kulazimisha kuwaongoza.
Wapinzani wapinga
"Kipindi hiki cha mpito kinapaswa kuwa cha kidemokrasia na chenye sura ya kiraia," imesema taarifa kutoka muungano wa vyama vya upinzani na makundi ya asasi za kiraia, ambazo zimeitisha maandamano katika uwanja mkubwa wa Place de la Nation, uwanja wa Taifa leo Jumapili, (02.11.2014).
"Mafanikio ya vuguvugu la umma - na hatimaye utawala wa mpito - ni ya wananchi na hayafai kutekwa na jeshi," taarifa hiyo imeongeza. Mzozo huo unaojitokeza katika taifa hilo masikini, lisilopakana na bahari unafuatiliwa kwa karibu na Marekani na mtawala wa zamani wa kikoloni Ufaransa , mataifa ambayo yamekuwa washirika wakubwa wa Compaore.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imeshutumu jeshi la Burkina Faso kutwaa madaraka na kulitaka kuhamisha madaraka haraka kwa maafisa wa kiraia. Marekani inaweza kuzuwia ushirikiano wake wa kijeshi iwapo itaamua kuwa yamefanyika mapinduzi.
Chini ya katiba ya Burkina Faso ya mwaka 1991 , spika wa bunge atachukua madaraka ya nchi iwapo rais atajiuzulu, akiwa na madaraka ya kuitisha uchaguzi katika muda wa siku 90. Hata hivyo , jeshi limelivunja bunge na kuifuta katiba. Katika taarifa iliyotolewa na viongozi wa jeshi baada ya kukutana na kumteua Zida kushika madaraka, wamesema muundo na kipindi cha mpito vitaamuliwa kwa mashauriano na sekta zote za jamii.
Majeshi yanayomuunga mkono Zida yamekuwa yakishika doria katika mitaa ambayo imekuwa tulivu mjini Ouagadougou jana Jumamosi kufuatia tangazo lake majira ya asubuhi kwamba anachukua madaraka ya nchi ili kuepuka taifa hilo kutumbukia katika machafuko makubwa na kuhakikisha hatua za mpito kuelekea katika demokrasia.
Marekani na Umoja wa Afrika
"Haya si mapinduzi lakini ni vuguvugu la umma ," Zida amesema, . "Natoa heshima kwa wahanga wa vuguvugu hili na natoa heshima zangu kwa watu wa nchi hii waliojitoa muhanga." Ametoa wito kwa Umoja wa Afrika na jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS kuonesha uungaji wao mkono wa kipindi cha mpito.
Lakini , katika taarifa yenye maneno makali, Umoja wa Afrika pia umelitaka jeshi kukabidhi madaraka kwa maafisa wa kiraia. Taarifa hiyo imesema baraza la usalama na amani la Umoja huo wenye wanachama 54 ambalo huweka vikwazo kwa ukiukaji wa hatua za demokrasia , litajadili hali hiyo kesho Jumatatu(03.11.2014).
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri : Bruce Amani.