1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Sudan Kusini lamuongezea muda Rais Kiir

25 Machi 2015

Bunge la Sudan Kusini limepiga kura kumuongezea muda zaidi Rais wa nchi hiyo, Salva Kiir na hivyo kuondoa uwezekano wa kufanyika uchaguzi mwaka huu, katika nchi hiyo inayokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/1ExD8
Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini, Salva KiirPicha: Reuters

Zaidi ya theluthi-mbili ya wabunge wa Sudan Kusini jana wameupitisha uamuzi wa kumuongezea Rais Kiir muda wa miaka mitatu zaidi madarakani, hatua ambayo serikali imesema ni muhimu kwa ajili ya amani na utulivu nchini humo, wakati uasi unaoongozwa na aliyekuwa makamu wa rais, Riek Machar ukiendelea.

Mwenyekiti wa Kamati ya habari ya bunge, Thomas Kundu, amesema wanaamini kuwa muda huo wa miaka mitatu utatoa nafasi ya kupatikana kwa amani, ili utaratibu wa zoezi la kuhesabu watu uweze kufanyika, hatua itakayochangia kufanyika kwa uchaguzi huru na wa haki.

Spika wa Bunge la Sudan Kusini, Manasseh Rundial, amesema bunge hilo pia limejiongezea muda wa miaka mitatu zaidi. Amesema marekebisho hayo yalianzishwa na Rais Kiir na leo anatarajiwa kuidhinisha uamuzi huo uliopitishwa na bunge.

Kiongozi wa waasi, Riek Machar
Kiongozi wa waasi, Riek MacharPicha: Reuters

Uamuzi huo umekosolewa

Hata hivyo, hatua hiyo imekosolewa vikali na wafadhili wa kimataifa, wapinzani pamoja na vyama vya kiraia, ambao wamesema kura yoyote inayopigwa wakati nchi hiyo iko katikati ya mzozo, haikubaliki. Mbunge wa upinzani, Onyoti Adigo, amesema kura hiyo inataka kuendelea kumuweka madarakani Rais Kiir kwa muda mrefu zaidi.

Adigo alipiga kura ya hapana kuupinga uamuzi huo. Amesema watu hawakushirikishwa, ndiyo maana wanaupinga uamuzi huo. Badala yake wapinzani wamezitaka pande zinazohasimiana kuhakikisha zinafikia makubaliano ya amani na kumaliza mapigano ambayo yanazidisha mzozo wa kibinaadamu nchini humo.

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea kusikitishwa kwake na pande zinazohasimiana nchini Sudan Kusini kushindwa kufikia makubaliano ya amani. Wanachama 15 wa baraza hilo jana walilaani vikali hatua ya pande hizo kurudia tena kukiuka mpango wa kusitisha makubaliano uliosainiwa na Rais Kiir na mpinzani wake, Machar.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Getty Images/A. Burton

Rais wa Baraza hilo, Francois Delattre, ambaye pia ni Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja wa Mataifa, amesema kutokana na hali iliyopo Sudan Kusini, wanafikiria kuweka vikwazo.

Vikwazo vya silaha au kwa watu binafsi

''Vikwazo hivyo vinaweza kuwa vya silaha pamoja na vikwazo binafsi kwa wajumbe wa pande zote ambao wanaohusika na kutishia usalama na utulivu wa Sudan Kusini,'' alifafanua Delattre.

Mwanzoni mwa mwezi huu baraza hilo liliidhinisha azimio la kuanzisha vikwazo kwa serikali ya Sudan Kusini. Kamati husika itakutana leo kwa mara ya kwanza kuangalia uwezekano wa kuanzishwa vikwazo hivyo.

Mjumbe wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa, Francis Deng ameliambia baraza hilo, anaamini kuwa mara chache sana vikwazo vimesaidia kuleta suluhisho lililokusudiwa, na badala yake vimekuwa vikichochea ghasia zaidi.

Watoto wa Sudan Kusini wakienda kuchukua msaada wa chakula
Watoto wa Sudan Kusini wakienda kuchukua msaada wa chakulaPicha: Nichole Sobecki/AFP/Getty Images

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni moja wameyakimbia makaazi yao tangu kuanza kwa mapigano kati ya Rais Kiir na aliyekuwa makamu wa rais, Machar, mwishoni mwa mwaka 2013.

Ama kwa upande mwingine, madaktari wasio na mipaka wamesema mripuko wa silaha ambazo zimerundikwa kwenye kontena katika mji unaodhibitiwa na waasi wa Thar Jath, Sudan Kusini, umesababisha vifo vya watu saba, akiwemo mvulana wa miaka 14.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,AFPE,DPAE,RTRE
Mhariri: Gakuba Daniel