1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Utawala wa sheriaAmerika ya Kaskazini

Marekani yapitisha muswada wa kuiwekea vikwazo ICC

7 Juni 2024

Bunge la Marekani limepitisha siku ya Jumanne muswada utakaopelekea Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC kuwekewa vikwazo kutokana na hatua ya Mahakama hiyo kuomba waranti wa kukamatwa kwa maafisa wakuu wa Israel.

https://p.dw.com/p/4gfFw
Washington - Bunge la Marekani
Jengo lililopo Bunge la Marekani mjini WashingtonPicha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Muswada huo unaotoa uwezekano wa  Mahakama ya ICC  kuwekewa vikwazo umepitishwa kwa kura 247 dhidi ya 155 za wale walioupinga.

Kupitishwa kwake ni hatua ya kwanza ya bunge la Congress kuonesha kutoridhishwa kwake na hatua ya mahakama hiyo ya kimataifa kutaka waranti wa kukamatwa kwa viongozi wa Israel.

Hatua hii ya Bunge la Marekani imedhihirisha kwa mara kwanza mgawanyiko baina ya wanasiasa nchini humo kuhusu uungwaji mkono kwa Israel katika vita vyake dhidi ya kundi la Hamas katika  Ukanda wa Gaza.

Licha ya kuwa muswada huo ulitarajiwa kupitishwa katika Bunge hilo la Marekani lakini umewavutia wabunge wachache wa chama cha Democratic, jambo ambalo huenda likatatiza nafasi yake ya kupita katika Baraza la Senati. Hata Ikulu ya White House inaupinga muswada huo ikisema umechupa mipaka.

Je, muswada huo una nafasi gani kuwa sheria?

The Hague | Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC mjini The Hague, UholanziPicha: Peter Dejong/AP/dpa/picture alliance

Wawakilishi wa vyama vya Republican na Democratic waliomo kwenye Kamati inayohusika na mambo ya nje katika Bunge hilo wamesema mswada huo una nafasi ndogo mno wa kuidhinishwa kuwa sheria na wakahimiza mazungumzo zaidi na Ikulu ya White House wakisema itakuwa bora kwa Baraza la Congress kuungana dhidi ya Mahakama hiyo ya ICC yenye makao yake mjini The Hague.

Soma pia: ICC na wafanyakazi wake walengwa na visa vya ujasusi

Mike McCaul, Mwenyekiti, Kamati hiyo ya Mambo ya Nje ya Bunge amesema:

"Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imevuka mamlaka yake na kuwacha historia ya hatari kwa kuomba vibali vya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant, sambamba na magaidi wa Hamas. Ninataka kuwa muwazi: kesi dhidi ya Israel haina msingi."

Mswada huo unalenga kuwawekea vikwazo vya kiuchumi na sheria kali za maombi ya visa kwa watu binafsi, majaji  na familia zao ambao watahibitika kuwa na mafungamano na  ICC.

Gaza I Mashambulizi ya Israel huko Bureij.
Wapalestina wakishuhudia uharibifu uliosababishwa na mashambulizi ya Israel huko GazaPicha: Hashem Zimmo/ZUMAPRESS/picture alliance

Hayo yakijiri, vita vinaendelea kurindima huko Gaza ambako Israel imeendeleza mashambulizi yake leo Jumatano na kusema sasa wameanzisha rasmi operesheni katikati mwa Gaza.

Wakati huo huo, timu ya wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar wanapanga kuanza tena mazungumzo yaliyokwama kuhusu makubaliano ya usitishwaji mapigano na kuachiliwa kwa mateka. Mzozo huu ulioanza Oktoba 7 mwaka jana baada ya shambulizi la  Hamas  kusini mwa Israel tayari limesababisha vifo vya Wapaletina zaidi ya 36,000, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas ambayo imeorodheshwa na Umoja wa Ulaya, Marekani, Ujerumani na mataifa kadhaa ya Magharibi kama kundi la kigaidi.