1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga na Premier League uwanjani

24 Aprili 2009

Wolfsburg na Manchester united zaongoza kileleni.

https://p.dw.com/p/Hdhk
Grafite (kulia) wa WolfsburgPicha: picture-alliance / Pressefoto ULMER / Lukas Coch

Katika Bundesliga mwishoni mwa wiki hii,viongozi wa Ligi -Wolfsburg wakiongoza kwa pointi 3,wanaazimia jumamosi hii kutanua mwanya wao kileleni kwa pigo kali mara hii usoni mwa Energie Cottbus. Mabingwa Bayern Munich wanaonyatia nafasi ya pili na nyuma pointi 3 ,wana miadi na Schalke .Mancherster United nayo imepanua juzi uongozi wake wa Premier League huko Uingereza kwa pointi 3 na jioni ya leo, wanakutana na Tottenham Hotspur wakati mahasimu wao Liverpool wana miadi na Hull City.

Macho yanakodolewa kesho mkenya Martin Lel kujua iwapo atatamba tena kama mwaka jana katika mbio za London marathon ?

Tukianza na ligi ya Ujerumani-Bundesliga,Wolfsburg, timu ya kocha Felix Magath, imeshinda mapambano 10 yaliopita na ushindi wa 11 kesho Jumapili nyumbani mwa Energie Cottbus,utaweka rekodi ya msimu katika Bundesliga. Wolfsburg hapo itavunja rekodi ya kushinda mara 10 iliowekwa msimu mmoja na Borussia Moenchengladbach,1987.

Ikiwa Wolfsburg pia itashinda mapambano 5 yajayo,sio tu itavikwwa taji la ubingwa msimu huu bali pia itaweka rekodi ya kushinda mara 16 mfululizo isiowahi kuwekwa katika Bundesliga. Kwani, itavunja ile ya mapambano 15 iliowekwa na mabingwa Bayern munich,2005. Wolfsburg kabla kuingia uwanjani kesho, inaongoza Bundesliga kwa pointi 57 ikifuatwa na Bayern Munich na Hamburg zenye pointi 54 wakati hertha Berlin ina pointi 52 na stuttgart 51.

Munich ikinyatia nafasi hiyo ya pili leo wanatamba nyumbani wakiikaribisha Schalke iliomaliza misukosuko yake ya karibuni na sasa inarudi kutamba. Munich haimudu kupoteza pointi ,kwani taji la Ujerumani ndilo kifuta-machozi pekee msimu huu baada ya kutimuwa nje ya champions league na FC Barcelona.

Kama Munich,Hamburg yenye miadi leo na Borussia Dortmund , haitamudu nayo kupoteza leo pointi ikiwa inataka kuvaa taji. Hamburg ilitapia mataji 3 msimu huu,kwani mbali na Bundesliga wametazamia kucheza finali ya Kombe la Ujerumani,lakini majirani zao Bremen waliitoa hamburg juzi kwa changamoto za mikwaju ya penalty.Sasa tumaini lao ni taji la bundesliga na la Kombe la UEFA ambao Bremen pia ni kizingiti.

Changamoto nyengine jioni hii ni Stuttgart ikipambana Frankfurt.Bayer Leverkusen inacheza na Karlsruhe wakati bremen inakusudia kutamba nyumbani mbele ya Bochum.Hannover inaikaribisha nyumbani FC Cologne inayoania pointi 3 kujiokoa kuteremshwa daraja ya pili.Kesho pia ni changamoto baina ya B.Moenchengladbach na Arminia Bielefeld.

Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Manchester United ilikaza kamba kileleni juzi ilipoizaba Portsmouth mabao 2-0 wakati Chelsea, ilimudu suluhu 0:0 na Everton.

Manchester United ina miadi jumam osi hii na Tottenham Hotspur wakati chelsea inaitembelea West ham united.Liverpool inaitembelea Hull City.

Mbali na changamoto hizo za Premier League, jumapili ni zamu tena ya mbio za London marathon.Mkenya Martin Lel ,bingwa wa mwaka jana atazamiwa tena kuwika.taarifa kutoka waandazi wa mbio hizo zimesema mkenya huyo mwenye umri wa miaka 30 sasa ni fit baada ya kuugua maumivu pajani.

Kwa upande wa wanawake, bingwa wa olimpik Constantina Dita atajaribu kushinda London marathon kesho kwa mara ya kwanza baada ya majaribio yake 8 kushindwa.Akiwa na umri wa miaka 39,hatajali umri wake, bali atategemea umaarufu wake uliompatia taji la Olimpik.Bingwa mara 2 wa dunia Catherine Ndereba ,aliemaliza wapili nyuma ya Dita katika michezo ya Olimpik ya Beijing ,anadai nae umri si kitu.Anaahidi nae kutamba kesho.

Muandishi:Ramadhan Ali

Mhariri: Othman Miraji