1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS-Jumia ya Ulaya yaunga mkono uteuzi wa Rais mpya wa benki ya Dunia.

31 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFRe

Jumuia ya Ulaya imeunga mkono uteuzi wa Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani Paul Wolfowitz,katika nafasi ya Rais wa Benki ya Dunia.Uteuzi wake umeibua shutuma nyingi kutoka sehemu mbalimbali duniani,kutokana na Bwana Wolfowitz kutokuwa na uzoefu wa masuala ya maendeleo na pia shutuma nyingine zilielekezwa kutokana na kuwa kinara wa maandalizi ya vita vya kuivamia Iraq.

Zaidi ya vikundi 1,300 vinavyojihusisha na utoaji misaada na vingine vya maendeleo katika nchi za Ulaya,vimekuwa vikipinga uteuzi wa Bwana Wolfowitz kuwa Rais wa Benki ya Dunia.

Jana Bwana Wolfowitz alikuwa mjini Brussels kwa mazungumzo na viongozi wa Jumuia ya Ulaya.

Taarifa kutoka kwa Wanadiplomasia wa Umoja wa Ulaya,zimesema wataunga mkono uteuzi wa Bwana Wolfowitz,lakini watataka naibu wake atoke katika nchi ya Ulaya.

Bodi ya Benki ya Dunia inapiga kura leo kumchagua mtu atakayechukua nafasi ya James Wolfensohn,ambaye anastaafu baada ya kuitumikia Benki ya Dunia katika nafasi ya Urais wa Benki ya Dunia kwa muongo mmoja.