Brahimi akutana na Muallem
30 Oktoba 2013Muallem alisema hayo wakati akizungumza na mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Mataifa ya Kiarabu, Lakhdar Brahimi, ambaye anajaribu kutafuta uungwaji mkono wa mazungumzo ya amani mjini Geneva.
Syria itashiriki katika mazungumzo ya Geneva katika msingi wa haki kamili za Wasyria kuchagua mustakabali wao wa kisiasa, kuwachagua viongozi wao na kutupilia mbali aina yoyote ya uingiliaji kutoka nje, amesema waziri huyo wa mambo ya kigeni Walid Muallem.
Pia amesema kuwa maelezo yote juu ya hali ya baadaye ya nchi hiyo, hususan matamshi kutoka mjini London, yanakiuka haki ya watu wa Syria.
Hii ni kwa mujibu wa mkutano uliofanyika Oktoba 22 wa kile kinachojulikana kama "Marafiki wa Syria", kundi la mataifa, ambayo yanaunga mkono upinzani nchini Syria.
Katika mkutano huo, mataifa ya magharibi na yale ya Kiarabu yalikubaliana na viongozi wa upande wa upinzani kuwa Assad hana nafasi katika uongozi wa hapo baadaye nchini humo kama alivyoeleza waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, William Hague.
"Assad hatakuwa na wajibu wowote katika utawala mpya wa Syria."
Lakhdar kukutana na Assad
Leo hii (30.10.2013)mjumbe wa Umoja wa Mataifa na mataifa ya Kiarabu Lakhdar Brahimi atakutana na rais wa Syria Bashar al-Assad mjini Damascus, zimesema duru za kidiplomasia. Utakuwa ni mkutano wa kwanza kati ya viongozi hao wawili tangu pale Brahimi alipozuru nchini humo Desemba mwaka jana.
Wakati huo huo, karibu Wasyria 2,000 wamekimbia kutoka katika wilaya iliyokumbwa na mapigano mjini Damascus ya Moadamiyeh jana kwa msaada wa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wakati wa muda mfupi wa kusitisha mapigano, ikiwa ni matokeo ya makubaliano ambayo ni ya nadra kati ya majeshi ya serikali na waasi katika hatua ya kuepusha hali mbaya ya mzozo wa kibinaadamu.
Njaa na magonjwa
Hatua hiyo imewezekana baada ya ripoti za ukosefu wa chakula na njaa pamoja na magonjwa katika kitongoji cha magharibi mwa mji huo baada ya miito ya jumuiya ya kimataifa.
Nalo shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, limethibitisha jana kuwa umezuka ugonjwa wa polio katika nchi hiyo iliyokumbwa na vita, ambayo ilikuwa haina ugonjwa huo tangu mwaka 1999, na shirika hilo limesema linahofia kusambaa kwa ugonjwa huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/ape
Mhariri: Josephat Charo