1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken asisitiza makubaliano ya usitishaji vita Gaza

Angela Mdungu
18 Septemba 2024

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema usitishaji wa vita katika mzozo wa Israel na Hamas kwenye Ukanda wa Gaza, ndiyo njia bora zaidi ya kukomesha machafuko yasiendelee Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/4knxx
Blinken aizuru Misri kutafuta usuluhishi vita vya Gaza
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken akiwa na Rais wa Misri Abdel-Fattah al-SisiPicha: Egyptian Presidency/Xinhua/picture alliance

Akiwa ziarani Cairo nchini Misri, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema moja ya masuala muhimu yaliyojadiliwa kwenye ziara hiyo ni umuhimu wa kufanikisha upatikanaji wa makubaliano ya kusitisha vita Gaza, kati ya Israel na kundi la Hamas.

Mbele ya mkutano na waandishi wa habari, Blinken ameeleza kuwa kupatikana kwa makubaliano hayo kutasaidia ku shughulikia utulivu katika ukanda huo.

Soma zaidi: Hezbollah yaapa kulipa kisasi mashambulizi dhidi ya Lebanon

Katika mkutano huo aliongozana na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Misri Badr Abdelatty ambaye alisema kuwa, "Tumejadili kuhusu mgogoro mbaya katika Ukanda wa Gaza na tumekubaliana na msimamo wa pamoja kuhusu hitaji la haraka la kupata makubaliano ya kusitisha vita na kuzuwia umwagaji damu wa watu wa Palestina. Tumezungumzia umuhimu wa makubaliano yatakayosaidia kuachiliwa kwa mateka na wafungwa yanayohakikisha pia kuna upatikanaji wa misaada ya kitabibu na kiutu kwa wakazi wa Ukanda wa Gaza".

Kutokana na mkutano na Blinken, ofisi ya Rais wa Misri Abdel Fatah al Sisi imesema kuwa wawili hao wamejadili njia za kuongeza juhudi kati ya Misri, Qatar na Marekani ili wapige hatua katika mazungumzo ya usitishaji vita na kubadilishana wafungwa na mateka.

Kwingineko, nchini Lebanon, idadi ya waliouwawa baada ya vifaa vya mawasiliano vya wanagambo wa Hezbollah kulipuka kwa pamoja Jumanne katika maeneo kadhaa imefikia watu 12. Takwimu hizo zimetolewa na Waziri wa Afya wa Lebanon, Firass Abiad. 

Viongozi mbalimbali walaani shambulio lililofanywa Lebanon

Naye Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema washirika wa magharibi wa Israel wanapaswa kuona haya baada ya vifaa vya mawasiliano vya wanamgambo wa kundi la Hezbollah kulipuka. Iran inaishutumu Israel kuwa ndiyo iliyohusika na shambulio hilo. Amesema Marekani na washirika hao wanaunga mkono uhalifu, na mauaji ya raia.

IRais wa Iran Masoud Pezeshkian katika moja ya hotuba zake Tehran
Rais wa Iran Masoud PezeshkianPicha: Morteza Nikoubazl/NurPhoto/picture alliance

Soma zaidi: Hezbollah yailaumu Israel kwa mashambulizi ya kieletroniki Lebanon

Naye  Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, amesema waliohusika na shambulio hilo baya nchini Lebanon wanapaswa kuwajibishwa. Amelielezea shambulio hilo kuwa la kushtusha na kuwa madhara yake kwa raia hayakubaliki.

Kwa upande wake Mkuu wa sera za kigeni Josep Borell amelaani kitendo hicho cha kulipuliwa kwa vifaa vya mawasiliano nchini Lebanon. Borell amesema hata kama mashambulizi hayo yanaonekana kuwalenga wahusika, yalikuwa na madhara kwa raia wakiwemo watoto.