1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden anahofia 'hasara kubwa ya maisha'

30 Septemba 2022

Rais wa Marekani Joe Biden anapanga kuzuru Florida baada ya kukumbwa na kile kinachohofiwa kuwa mojawapo ya vimbunga vilivyosababisha vifo vya watu wengi zaidi katika historia ya jimbo hilo.

https://p.dw.com/p/4HYzM
USA Hurrikan Ian | Fort Myers, Florida
Picha: Wilfredo Lee/AP Photo/picture alliance

Akizungumza katika makao makuu ya Shirika la Usimamizi wa Dharura (FEMA) ambalo limekuwa likiandaa misaada ya serikali kwa maafa ambayo yamesababisha uharibifu katika jimbo la kusini mwa peninsula, Biden amesema anahofia 'hasara kubwa ya maisha' kutokana na kimbunga Ian.

soma Kimbunga Ian chapiga Cuba

Takriban vifo sita vimeripotiwa, lakini idadi hii inatarajiwa kuongezeka huku waokoaji wakienea katika maeneo yaliyoathiriwa.

Gavana wa Florida Ron DeSantis amewaambia wanahabari kwamba jimbo hilo halijawahi kukabiliwa na dhoruba kubwa kama hiyo.

Kituo cha Kitaifa kinachoshughulikia masuala ya Vimbunga (NHC) kilitoa onyo katika ukanda wa pwani wa Carolina Kusini, wakati kimbunga Ian kikielekea kaskazini zaidi kwa upepo unaovuma kwa kasi ya mita 70 kwa saa.

soma Kimbunga chauwa zaidi ya watu 70 Marekani

Biden aahidi misaada zaidi

USA, Washington | Joe Biden bei der FEMA
Picha: Bonnie Cash/Pool/CNP/MediaPunch/picture alliance

Rais Biden ameidhinisha tamko la dharura na kuagiza ufadhili wa misaada katika kaunti zilizoathiriwa na dhoruba.

"Tunajua familia nyingi zinaumia. Wengi, wameumia. Na nchi yetu nzima inaumia nao .Tumeona migogoro mingi. Lakini Florida, leo ni ndio kitovu. Tunaendelea kuona mvua mbaya, majanga ya dhoruba. Barabara na nyumba zimejaa maji. Tunaona mamilioni ya watu wasio na nguvu na maelfu wakiteseka, shuleni na katika vituo vya jamii. Wanashangaa nini kinaendelea? Ujumbe wangu kwa watu wa Florida, na nchi nzima ni wakati kama huu, Amerika inakusanyika. Tutaungana kama timu moja, kama Amerika moja. Biden alisema.

soma Hasara zaongezeka kutokana na majanga ya mabadiliko ya hewa

Dhoruba hiyo ilibadilisha ufuo wa kusini-magharibi wa Florida, ulio na fukwe za bahari, miji ya pwani kuwa eneo la maafa wakati  kimbunga Ian kilipopiga maji ya bahari kwenye nyumba zilizo karibu na maji.

Kanda za video zilionyesha maji ya mafuriko yakiingia kwenye nyumba zilizo karibu na ufuo, barabara zilizo chini ya maji na kubeba magari.

Wakaazi katika maeneo yaliyoathirika zaidi kama Venice, iliyoko katika kaunti ya Sarasota takriban kilomita 120 kusini mwa Tampa, wanaendelea kutafuta familia na marafiki huku waokoaji wakifanya kazi ya kuwafikia watu waliokwama katika nyumba zilizofurika.

Utafutaji wa huo ulifanywa kuwa mgumu zaidi kwani huduma za simu za rununu kwa muda hazikua zikipatikana.

 

DW/Reuters