Bei za Hisa Ulaya na Asia zashuka Ijumaa
3 Oktoba 2008Bei ya hisa ilishuka leo Ijumaa katika masoko ya hisa barani Ulaya na Asia wakati ikiwa inasubiriwa kura ya mara ya pili katika baraza la wawakilishi la Marekani kuhusu muswada wa serikali ya Marekani wa dola billioni 700 wa kuupiga jeki mfumo wa fedha wa Marekani.
Wasiwasi unatokana na hofu ya kuwa huenda ukakataliwa na baraza hilo kama ilivyokuwa,mapema wiki hii japo ulipasishwa juzi na baraza la Senate ukiwa umefanyiwa marekebisho.
Baraza la wawakilishi la Marekani ndio lina kadi ya turufu kuhusu mpango wa kuunusuru sio tu mfumo wa fedha wa Marekani unaoyumbayumba lakini pia na wa karibu dunia nzima ambao umeathirika na yanayotokea nchini Marekani.
Baraza hilo linapiga kura Ijumaa, kwa mara nyingine tena,baada ya kuukata muswaada huo jumatatu na hivyo kusababisha kuporomoka kwa bnei za hisa katika masoko mbalimbali ya hisa duniani, hususan barani Ulaya pamoja na Asia.
Inatarajiwa kuwa huenda baraza la wawakilishi, mara hii, litaupigia kura ya ndio mpango huo kwa sababu mbili: moja umefanyiwa marekebisho, na pia kuwa mpango huu mpya umepasishwa na baraza la senate juzi.
Licha ya hoja ya kuwa muswada huo umepasishwa na baraza la senate juzi,kwa hivyo utakubaliwa na baraza la wawakilishi, haijaondoa wasiwasi miongoni mwa wawekezaji.
Hoja yao ni kuwa ikiwa mara ya kwanza baraza hilo liliukataa na hivyo linaweza kufanya vivyo hivyo mara hii.Wasiwasi huo umepelekea bei za hisa kuporomoka katika masoko ya hisa duniani leo ijumaa.
Mapema Ijumaa masoko ya Ulaya yalishuhudia kushuka kwa bei za hisa.Hisa katika soko la jiji la London zilishuka kwa 0.60% ,Paris 0.48% na Frankfurt kushuka kwa kiasi cha asili mia 0.08% .
Yeye kuu wa Banki kuu ya Ulaya Jean-Claude Trichet amesema kuwa uchumi wa mataifa ya ulaya yanayotumia sarafu ya Euro kwa njia moja au nyingine unakabiliwa na athari za mgogoro wa kifedha wa Marekani.
Masoko matatu ya hisa ya bara la Ulaya alhamisi yaliweza kupandisha thamani ya hisa zake kwa 2%.
Hali ya sasa ya mparaganyiko katika mfumo wa fedha bila shaka itakuwa ajenda mojawapo ya mkutano wa Jumamosi utakaofanyika mjini Paris Ufaransa baina ya viongonzi wa mataifa manne yenye uchumi mkubwa katika Umoja wa Ulaya.
Mataifa hayo ni Ujeruamni, Uingereza, Ufaransa pamoja na Italy.Kumekuwa na pendekezo kuwa Umoja wa Ulaya uunde mpango kama ule wa Marekani wa kuupiga jeki mfumo wa fedha. Hata hivyo Ujerumani inapinga wazo hilo.
Hayo yakiwa yanaendelea wasiwasi unaendelea kusababisha kushusha bei za hisa kwingineko kama vile Tokyo,Hongkong,Seol na Sydney.
Na hivyo inasubiriwa kuwa huenda baraza la wawakilishi la Marekani litaleta tabasamu katika ulimwengu wa sekta ya fedha.