1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaikaanga Hertha na kujiimarisha kileleni

24 Januari 2022

Vinara wa Bundesliga Bayern Munich walituma ujumbe mzito kwa wapinzani wao wa karibu Borussia Dortmund baada ya kuwabamiza Hertha Berlin 4 – 1 katika mechi ya Jumapili 23.01.2022

https://p.dw.com/p/460Zf
Fußball Bundesliga | Hertha BSC - FC Bayern München
Picha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Ushindi huo mnono ulirejesha mwanya wa pointi sita dhidi ya Bayern na Dortmund ambao walikuwa wameupunguza kwa pointi tatu tu kufuatia ushindi wao wa Jumamosi wa 3 – 2 dhidi ya TSG Hoffenheim.

Ni kichapo cha tatu mfululizo cha nyumbani kwa Hertha ambao waliondolewa katika Kombe la Shirikisho na watani wao Union Berlin kwa kufungwa 3 -2.

Mapema jana, RB Leipzig waliendelea na matokeo yao mazuri kwa kupata ushindi wa 2 – 0 dhidi ya Wolfsburg, ambao sasa wamecheza mechi tisa za Bundesliga bila kushinda hata moja.

Deutschland Bundesliga | TSG 1899 Hoffenheim vs Borussia Dortmund | Tor (0:1)
Haaland aliumia katika mechi dhidi ya HoffenheimPicha: Uwe Anspach/dpa /picture-alliance

Leipzg wameshinda mechi zao nne za mwisho katika mashindano yote na wamepanda hadi nafasi ya sita kwenye ligi. Kichapo hicho cha karibuni kinaongeza mbinyo kwa kocha wa Wolfsburg Florian Kohfeldt, ambaye alichukua usukani kutoka kwa Mark van Bommel aliyefutwa kazi mwishoni mwa Oktoba.

Mkurugenzi wa spoti wa Wolfsburg Marcel Schaefer amesema watashirikiana kwa pamoja na kuwa Kohfledt atakuwepo kuongoza kikosi kwa mechi ifuatayo dhidi ya washika mkia Gruether Fuerth. Dortmund wana pengo la pointi nane dhidi ya Bayer Leverkusen waliowafumua Augsburg kwa mabao 5-1.

Union Berlin wameingia katika nne bora baada ya kuwafunga Borussia Moenchegladbach 2 – 1 matokeo ambayo yalimuongezea mbinyo kocha Adi Huetter.

Gladbach walihitaji pointi tatu, wakiwa wameshinda tu mechi moja kati ya nane za mwisho katika ligi na kuondolewa katika kombe la DFB na Hanover.

Ushindi wa Freiburg wa 2 – 0 dhidi ya majirani zao Stuttgart umewaweka nafasi ya tano pointi moja nyuma ya Union. Washika mkia Greuther Fuerth ilipata ushindi wa 2 – 1 dhidi ya Mainz, wakati Cologne walitoka sare ya 2 2 na Bochum.

afp, reuters, dpa, ap