1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern waonyesha makali yao tena, wapunguza pengo nyuma ya Dortmund

13 Machi 2012

Bayern Munich walirejea baada ya kipigo cha Bayer Leverkusen kwa kuwasambaratisha Hoffenheim magoli saba kwa moja mwishoni mwa juma.

https://p.dw.com/p/14JVr
Torjubel zum 6-0: Torschuetze Mario GOMEZ (FC Bayern) /re. mit Franck RIBERY (FC Bayern) /li. und Arjen ROBBEN (FC Bayern) /Mitte. Fussball 1.Bundesliga: FC Bayern Muenchen - TSG 1899 Hoffenheim, Muenchen, 10.03.2012 -- Football, Soccer 1st. German Bundesliga/ Division: FC Bayern Munich vs. 1899 Hoffenheim , Munich, March 10, 2012 --
Fussball 1. Bundesliga 25. Spieltag, FC Bayern Muenchen gegen TSG 1899 Hoffenheim in Allianz-Arena MuenchenPicha: picture alliance/augenklick/GES

Mario Gomez aliongoza ufungaji alipotia kimiani magoli matatu, huku Arjen Robben akifunga mawili kabla ya Toni Kroos na Franck Ribery kugawan magoli mengine. Mchezaji mwingine wa Bayern aliwapa zawadi Hoffenheim ya kufuta machozi wakati Luis Gustavo alipojifunga bao mwenyewe.

Bayern, wa pili katika ligi, wana pointi 51 kutokana na mechi 25 na kupunguza pengo kwa alama tano na Borussia Dortmund baada ya viongozi hao kutoka sare ya kutofungana na Augsburg. Nambari tatu Borussia Moenchengladbach pia walitoka sare ya bila kufungana nyumbani kwa Freiburg na kuangusha pointi tatu nyuma ya Bayern.

Nchini Uingereza, Manchester United ilichukua usukani wa Premier League kwa mara ya kwanza tangu mwezi Oktoba wakati magoli mawili yake Wayne Rooney yalipowapa ushindi wa mbili nunge dhidi ya West Bromwich Albion, nao viongozi Manchester City wakishindwa goli moja kwa nunge na Swansea. Mabingwa hao wana pointi 67 na mechi kumi zilizosalia, alama moja mbele ya City walioongoza ligi kwa muda mrefu. Tottenham Hotspur wangali katika nafasi ya tatu na alama 53 licha ya kushindwa na Everton goli moja kwa nunge.

Redknapp ajitenga na ukufunzi wa timu ya taifa Uingereza

Meneja wa Tottenham Hotspurs, Harry Redknapp amejitenga na wadhifa wa ukufunzi wa timu ya taifa ya soka ya Uingereza, akisema ana furaha kuwa katika uwanja wa White Hart Lane na kudokeza kuwa kazi ya hiyo ya taifa inaweza kuchosha sana.

Spurs imesajili matokeo mema katika ligi ya Uingereza
Spurs imesajili matokeo mema katika ligi ya UingerezaPicha: AP

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 65 anayepigiwa upatu na wengi kuchukua wadhifa huo mahala pa Fabio Capello baada ya muitaliani huyo kujiuzulu mwezi uliopita. Mashabiki na vyombo vya habari wamekuwa wakimpigia debe Redknapp kama mtu anayeweza kuiongoza Uingereza katika fainali za euro 2012. Redknapp anasisitiza kuwa hana mkataba wowote kutoka shirikisho la Soka la Uingereza, FA, ambao wamempa Stuart Pierce kazi ya muda hadi pale watakapompata kocha wa mkataba mrefu. Wakati huohuo, inadaiwa kuwa Spurs wamempa mkataba mpya ulioimarishwa pamoja na bajeti kubwa ya kuwasajili wachezaji wapya.

Ligi ya Mabingwa Ulaya

Ligi ya mabingwa barani Ulaya - UEFA Champions League huenda ikawa na mojawapo ya orodha ya mchanganyiko kabisa ya robo fainali katika historia yake ya miaka 20 ikiwa timu nne ambayo ni miamba ya soka Ulaya zitashindwa kuimarisha mchezo wao katika michuano ya mkondo wa pili wa awamu ya 16 wiki hii.

APOEL Nicosia, timu ya kwanza kabisa ya Cyprus kuwahi kufika awamu ya maondowano katika dimba hili, na Benfica, ambayo siku zake njema barani Ulaya zilijiri katika miaka ya sitini, zilifuzu katika nane za mwisho wiki iliyopita pamoja na Barcelona na AC Milan.

Real Madrid, Bayern Munich, Inter Milan na Chelsea, ambayo ni mwakilishi wa pekee wa Uingereza aliyesalia, zinalenga kujiunga na zile zilizofuzu. Real Madrid watacheza Jumatano dhidi ya CSKA Moscow nyumbani Santiago Bernabeu baada ya kutekwa sare ya bao moja katika mkondo wa kwanza.Bayern ilifungwa moja kwa sifuri na FC Basel katika mkondo wa kwanza nchini Uswisi na sasa watacheza kesho nyumbani Ujerumani.

Real Madrid ni sharti wawashinde CSKA Moscow nyumbani Bernabeu
Real Madrid ni sharti wawashinde CSKA Moscow nyumbani BernabeuPicha: AP

Nao Inter Milan walishindwa na Marseille moja kwa nunge na watajizatiti katika mchuano wa kesho uwanjani San Siro. Chelsea walilazwa magoli matatu kwa moja na Napoli lakini Jumatano watakuwa nyumbani Stamford Bridge kujaribu kuyageuza matokeo hayo.

Mwanariadha Mkenya Pamela Jelimo ang'ara

Bingwa wa Olimpiki, Pamela Jelimo wa Kenya, amerejea tena kwa kishindo. Mwanariadha huyo aliweka muda wa kasi zaidi ulimwengni msimu huu aliposhinda dhahabu katika mashindano ya riadha ya ulimwengu ya kumbini, Uturuki. 

Jelimo alimaliza kwa muda wa1:58.83. Jelimo aliandika historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza mwanamke kushinda dhahabu katika mbio za mita mia nane. Ni Wilfred Bungei pekee aliyewahi kushinda dhahabu katika mitza mia nane lakini katika kitengo cha wanaume. Katika mbio za mita 3,000 kitengo cha wanawake, Mkenya Hellen Obiri alimshangaza bingwa mara tatu Muethiopia, Meseret Defar, baada ya kumaliza kwa muda wa 8:37.16 na kutwaa dhahabu. Defar na Gelete Burka walichukua fedha na shaba mtawalia.

Pamela Jelimo amekuwa nje ya mashindano kwa muda mrefu
Pamela Jelimo amekuwa nje ya mashindano kwa muda mrefuPicha: AP

Katika mbio za mita 3,000 kwa wanaume, kigogo Benard Lagat aliinyakulia Marekani medali ya dhahabu baada ya kuwapiku Wakenya Augustine Choge na Edwin Soi. Kenya ilipata jumla ya medali nne, dhahabu mbili, fedha moja na shaba moja na kumaliza ya nne nyuma ya Ethiopia ambao walikuwa na shaba moja zaidi.

Chisora akiri kuaibika

Katika ndondi bondia Dereck Chisora amekiri kuwa aliabika sana kutokana na tabia yake ya kuzozana hadharani mjini Munich mwezi uliopita. Chisora ameyasema hayo wakati akijiandaa kufika mbele ya Bodi ya Udhibiti wa Ndondi nchini Uingereza siku ya Jumatano (14.03.2012). Bondia huyo, mwenye umri wa miaka 28, mzaliwa wa Zimbabwe, huenda akapigwa marufuku katika mchezo huo na bodi hiyo kuhusiana na matukio ya kabla na baada ya pigano lake la uzani wa juu la kuwania taji la WBC dhidi ya Vitali Klitschko nchini Ujerumani tarehe 18 Februari.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP

Mhariri: Miraji Othman