Barua ya Abbas kwa Netanyahu
17 Aprili 2012Ingawa hakukuwa na tangazo rasmi juu ya mkutano huo, maafisa kutoka serikali ya Palestina walithibitisha kuwa wawili hao wangekutana siku ya Jumanne.
Afisa moja wa Israel alisema Waziri Mkuu Benjamini Netanyahu angerejelea wito wake wa kuanzisha tena mazungmzo ya amani pasipo kuweka masharti yoyote, na pia kutaka akutanishwe na rais wa mamlaka ya palestina, Mahmoud Abbas.
Ni juhudi mpya za utambuzi wa Taifa la Palestina?
Lakini barua hii kutoka kwa Abbas, ambayo Fayyad aliikabidhi kwa Netanyahu, inaweza kuwa juhudi mpya ya kufungua mazungumzo baina ya Israel na Palestina juu ya kutaka kutambuliwa kwa taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa. Juhudi za awali ziligonga mwamba mwaka uliopita baada ya kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa Marekani na Israel.
Mbunge kutoka palestina, Hanani Ashrawi alisema hili ni jaribio la mwisho kuonyesha kuwa wanafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanapata suluhisho la kuwa na mataifa mawili, na kuelezea matumaini ya kupata majibu ya kuridhisha. Lakini aliongeza kuwa kama hakutakuwa na majibu, wao wana mkakati wa nini kitafuata.
Wapalestina wanasema barua hii inaweza kuishtumu Israel kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake kulingana na mpango wa amani wa mwaka 2003 uliokubaliwa na pande zote, ambao unahusisha kusimamishwa kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika maeneo ya Wapalestina.
Pongezi na tahadhari
Serikali za mataifa ya nje zimekaribisha hatua hii ya Rais Abbas kumtumia barua Waziri Mkuu Netanyahu, lakini zimeonya juu ya matumizi ya lugha ya vitisho. Rais Barack Obama wa Marekani alimpigia simu rais Mahmoud Abbas mwezi uliopita na kumtahadharisha juu ya vitendo vya kichokozi.
Rais Abbas amesisitiza kuwa barua yake, ambayo imechukua wiki kadhaa kuiandaa, inalenga tu kuikumbusha Israel juu ya wajibu wake chini ya mipango ya muda ya amani.
Abbas aliliambia shirika la habari la palestina WAFA wiki iliyopita kuwa, njia zote zitatumika ukiachilia kufutwa kwa mamlaka ya Palestina au kuacha kutambua uhalali wa kuwepo kwa taifa la Israel. Abbas alisema hawalengi kuitenga Israel bali hawakubaliani na sera yake ya ulowezi.
Netanyahu alisema mustakbali wa makaazi hayo ya Waisrael ambayo yanalaumiwa na Wapalestina na jamii nzima ya kimataifa, utaamuliwa kwa kufanyika kwa mazungumzo ya amani.
Mazungumzo ya amani yaliyodhaminiwa na Marekani yalikwama mwaka uliopita baada ya Netanyahu kukataa matakwa ya Wapalestina ya kusogeza mbele muda wa usitishwaji wa ujenzi wa makaazi ya walowezi uliofanywa kwa maombi ya Marekani kuzivuta pande hizo kwenye mazungumzo.
Matumaini ya Wapalestina
Wapalestina wana imani kuwa barua hii itaeleza vizuri msimamo wao kabla ya kuanza kwa juhudi mpya za kupigania utambuzi wa taifa lao ndani ya Umoja wa Mataifa.
Baada ya juhudi zao za awali kugonga mwamba ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Wapalestina walikuwa wanatafakkari kudai haki yao katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambako wana uungwaji mkono mkubwa. Hata hivyo, ni Baraza la Usalama pekee ambako Marekani ina kura ya turufu, linaloweza kuruhusu uanachama kamilia wa Umoja wa Mataifa.
Muandishi:Iddi Ismail Ssessanga\RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu