Baraza la Usalama laiwekea vikwazo Dola la Kiislamu
16 Agosti 2014Wakati huo huo kuna ripoti kuwa wapiganaji wa Jihad wa Taifa la Kiislamu wameuwa wakaazi kadhaa katika maeneo yaliyozingirwa ya jamii ya Wayazidi.
Vyombo vya habari vya mataifa ya magharibi vimeripoti kuwa dazeni kadhaa za wanaume kutoka jamii ya imani ya Yazidi wameuwawa katika kijiji cha Kocho, kilomita 45 kutoka mji unaoshikiliwa na Wakurdi wa Sinjar.
Baadhi ya ripoti zinazungumzia kuhusu wakaazi kulazimishwa ama kubadilisha dini na kuwa Waislamu ama kuuwawa.
Wakati taarifa zaidi kuhusu tukio hilo la hivi karibuni hazijathibitishwa mara moja, mashambulizi ya aina hiyo hapo zamani yamesababisha jeshi la Marekani kuchukua hatua.
Marekani yashambulia
Rais Barack Obama wa Marekani amesema wiki ya kwanza ya mashambulizi ya anga yamevunja mzingiro huo katika milima ya Sinjar upande wa kaskazini ambako raia wamekuwa wakijificha kwa muda wa zaidi ya siku 10.
Marekani ilifanya mashambulizi zaidi ya anga jana Ijumaa , jeshi limesema, baada ya kupata taarifa kuwa magaidi ya Taifa la Kiislamu wanashambulia raia katika eneo hilo.
Wakati mashirika ya kutoa misaada yanajaribu kutoa misaada kwa mamia kwa maelfu ya watu waliokimbia makaazi yao kutokana na mashambulizi ya kundi hilo la Taifa la Kiislamu (IS) kaskazini mwa Iraq, mapigano yalianza tena.
Mjini New York, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lenye lengo la kulidhoofisha kundi hilo la Kiislamu nchini Iraq na Syria kwa kuzuwia uwezo wao wa fedha pamoja na kuingia kwa wapiganaji kutoka nje.
Na mawaziri wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana katika mkutano mjini Brussels kuwaunga mkono kwa silaha wapiganaji wa jimbo la Wakurdi nchini Iraq.
Wairaki na mataifa yenye nguvu duniani wakati huo huo wameeleza kufarijika kwao baada ya uamuzi wa Waziri Mkuu Nuri al-Maliki siku ya Alhamis kujiuzulu.
Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa nchini Marekani Susan Rice amesema ni " hatua nyingine kubwa kuelekea mbele" katika kuiunganisha Iraq, ambako wapiganaji wa Jihad wa taifa la Kiislamu wamekamata maeneo ya ardhi katika mashambulizi yao ya haraka na kinyama , na kuzusha hofu ya mauaji ya halaiki.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon pia ameikaribisha hatua hiyo muhimu ya Maliki na kutoa wito wa kuundwa kwa haraka serikali itakayojumuisha makundi yote kwa haraka , ili kukabiliana na masuala muhimu yanayoikabili nchi hiyo.
Mrithi wa Maliki
Uungwaji mkono kwa mrithi wa kiti cha Maliki , Haidar al-Abadi, umemiminika kutoka kila kona kutoka Iran hadi saudi Arabia.
Wakati wapiganaji wa Jihad walipoanza mashambulizi yao Juni 9, majeshi ya Wakurdi wa Peshmerga yalifanikiwa kuliko majeshi ya serikali yaliyorudi nyuma, lakini silaha zilizotengenezwa Marekani zilizoachwa nyuma na majeshi hayo ya serikali, zimesababisha kundi la IS kuwa na nguvu zaidi.
Wakosoaji wa Maliki wanasema anabeba baadhi ya jukumu kuhusiana na mzozo huo ambao umeifikisha nchi hiyo katika ukingo wa kuvunjika kutokana na kuendeleza sera za kimadhehebu ambazo zimesababisha kutengwa na kuingiza hamasa za imani kali kwa Wasunni ambao ni wachache.
Katika hatua nyingine ya mabadiliko ya hali ya mambo , makabila 25 ya Wasunni katika jimbo la magharibi la Anbar, ikiwa ni pamoja na baadhi ambao hapo kabla walikataa kufanyakazi pamoja na serikali inayoongozwa na Maliki , wametangaza juhudi za pamoja kuwaondoa wapiganaji wa IS.
"Mapinduzi haya yamekubaliwa na makabila yote ambayo yanataka kupambana na IS, ambalo limemwaga damu yetu," Sheikh Abduljabbar Abu Risha , mmoja kati ya viongozi wa juhudi mpya dhidi ya wapiganaji wa Jihad ameliambia shirika la habari la AFP.
Mkuu wa jeshi la polisi katika jimbo la Anbar, Meja Jenerali Ahmed Saddak amesema majeshi ya usalama yanaunga mkono hatua hiyo, ambayo ilianza alfajiri ya Ijumaa.
Mapigano yanaendelea hadi sasa, amesema, akisema kuwa wapiganaji 12 wameuwawa na kuongeza "hatutasita hadi ukombozi kamili wa Anbar."
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef