1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la mawaziri liko tayari kufanya kazi

P.Martin29 Juni 2007

Waziri Mkuu mpya wa Uingereza,Gordon Brown amesema atafanya mageuzi makubwa ya kisiasa.Kwa hivyo amelipanga upya baraza lake la mawaziri, akiwapa kipaumbele wanademokrasia vijana walio na bidii

https://p.dw.com/p/CB3C
Waziri Mkuu wa uingereza Gordon Brown na mkewe Sarah,nje ya makazi rasmi ya Downing St.10
Waziri Mkuu wa uingereza Gordon Brown na mkewe Sarah,nje ya makazi rasmi ya Downing St.10Picha: AP

Gordon Brown anataka mabadiliko,si katika ajenda yake ya kisiasa tu,bali hata kwenye baraza lake la mawaziri.Alipotangaza mawaziri wake siku ya Alkhamisi,ilidhihirika wazi wazi kuwa waziri mkuu mpya anafuata mkondo tofauti kabisa na mtangulizi wake Tony Blair.Isipokuwa kwa wizara ya ulinzi, ambako Des Browne amebakia na wadhifa wake,kote kwengine kuna mabadiliko.

Waziri mpya wa masuala ya nje,ni David Miliband ambae amechukuwa nafasi ya Bibi Margret Beckett. Miliband aliekuwa waziri wa mazingira,si nyota mpya tu katika chama cha Labour,bali ana msimamo mkali kuhusu suala la Irak.Wakati ambapo Beckett alitetea vita vya Iraq mpaka dakika ya mwisho, Miliband mara nyingi alieleza shaka zake kuhusu Iraq.Miliband alie na umri wa miaka 41,ni waziri wa nje kijana kabisa wa Uingereza,tangu miaka 30 iliyopita.Lakini yaonekana kuwa anajiamini. Miliband ameueleza wajibu wake mpya hivi:

“Changamoto za ulimwengu wa kisasa kwa maoni yangu zinahitaji diplomasia yenye subira na madhumuni maalum - ikisikiliza na kuongoza pia. Hayo ni maadili ambayo nitajaribu kuhimiza wakati wa kuiongoza wizara ya nje.“

Miliband si mwanasiasa anaetegemewa tu na wademokrasia wa kijamii,bali inasemekana kuwa ana mengi yanayofanana na Blair.Baadhi ya wanachama wa Labour walimtaka Miliband apambane na Gordon ili kuweza kupata mshindi dhahiri.Lakini Miliband hakutaka kujiingiza katika kinyangányiro cha kumrithi Blair.

Badiliko jingine katika baraza jipya la mawaziri limeshangaza.Tangu hapo awali ilijulikana kuwa waziri wa ndani wa zamani,John Reid hakutaka kubakia,lakini kuchaguliwa kwa Jacqui Smith kuiongoza wizara hiyo imeshangaza wengi.Kwani hii ni mara ya kwanza kabisa nchini Uingereza,kwa mwanamke kupewa wadhifa wa kuongoza wizara ya mambo ya ndani.Licha ya kwamba hajawahi kuwa waziri hapo kabla na hana uzeofu katika sekta ya usalama wa ndani na vita dhidi ya ugaidi,Bibi Smith amepokea wadhifa huo kwa furaha na matumaini.Amesema hivi:

„Siwezi kufikiria dhima au heshima kubwa zaidi ya kupewa dhamana ya kulinda mipaka yetu,jamii na umma wetu ili waweze kuendelea na maisha yao.“

Mbali na kuingiza nyuso mpya,Brown amewaleta wale anaowaamini katika baraza la mawaziri.Kama ilivyotazamiwa,Alistair Darling aliekuwa waziri wa biashara,sasa ni waziri mpya wa fedha,akiwa na sifa ya ujuzi na uaminifu.Na Ed Balls,alie mshauri wa karibu sana na Brown amepewa wizara ya elimu na hivyo anashika wadhifa ulio na umuhimu mkubwa katika serikali mpya ya Uingereza.

Kijana mwengine mwenye bidii,Alan Johnson amepewa kazi ngumu kabisa.Yeye,kama waziri mpya wa afya ndio atajaribu kufanya mageuzi mengi katika sekta hiyo.Sifa ya Johnson ni kwamba yeye ni mpangaji wa mikakati,alie na uwezo wa kuwaeleza wapiga kura sera za kisiasa.Je ataweza kujitokeza kama mwana-mageuzi wa sera za afya?

Kwa jumla yaonekana kuwa baraza jipya la mawaziri,limeshachukua hatua ya kwanza ya mabadiliko.