1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiAfrika

Baerbock afanya ziara Ivory Coast baada ya Senegal

17 Julai 2024

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema nchi yake haiwezi kuendeleza ushirikiano na Niger kutokana na ukosefu wa "imani" katika mahusiano na utawala wa kijeshi wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4iQb0
Annalena Baerbock (kushoto) akiwa na Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (kushoto) akiwa na Rais wa Ivory Coast Alassane OuattaraPicha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Kauli ya Baerbock ameitoa hapo jana alipowasili mjini Abidjan nchini Ivory Coast akitokea nchini Senegal. Lakini mnamo Julai 6 mwaka huu, Ujerumani ilikuwa tayari ilitangaza kuwa itasitisha operesheni katika kambi yake ya anga huko  Niger  na kuwaondoa wanajeshi wake 36 waliosalia nchini humo ifikapo Agosti 31.

Hata hivyo Baerbock amesisitiza kuwa Ujerumani haikusitisha utowaji wa misaada kwa Niger kwa sababu raia wa nchi hiyo hawahusiki na kilichotokea lakini akaelezea ni kwanini Ujerumani ilichukua uamuzi wa kujiondoa katika baadhi ya mataifa:

" Kwa upande mwingine tumeshuhudia kuwa, kutokana na jukumu la Urusi nchini Mali na sasa  nchini Niger, hatukuweza kuendelea na jukumu letu tulilochukua hapo awali, katika sekta ya usalama, idara ya polisi na pia mafunzo kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa MINUSMA. Ni hilo ni kwa sababu uaminifu uliokuwepo hapo awali haukuwepo tena."

Kikosi maalum cha kupambana na Ugaidi kutoka chuo cha kimataifa cha Jaqueville
Kikosi maalum cha kupambana na Ugaidi kutoka chuo cha kimataifa cha Jaqueville, Ivory CoastPicha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari, Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara alimueleza Baerbock kuwa ukosefu wa utulivu katika mataifa Sahel ni hatari pia kwa nchi jirani:

"Tungependa kuona nchi hizi zikipata misaada ya kibinadamu kadri iwezekanavyo, kwa sababu wananchi wanaihitaji. Pia tulitaja hatari zinazoweza kusababishwa na hali hii kwa Ivory Coast, hasa katika mpaka wa kaskazini. Kama unavyofahamu, tayari tunapokea zaidi ya wakimbizi 60,000 kutoka Burkina Faso, na huu ni mzigo mkubwa kwa uchumi wa Ivory Coast."

Juhudi za Ujerumani katika kukabiliana na ugaidi

Baerbock akihudhuria mafunzo yanayotolewa ili kupambana na ugaidi huko Jacqueville.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (kushoto) akihudhuria mafunzo yanayotolewa ili kupambana na ugaidi katika chuo cha kimataifa huko Jacqueville.Picha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Katika ziara yake huko Ivory Coast, Baerbock alihudhuria mchakato wa mafunzo kwa vikosi vya usalama na ulinzi katika chuo cha kimataifa cha kukabiliana na ugaidi  kilichopo katika mji wa Jacqueville takriban kilomita 35 kutoka mji mkuu Abidjan. Ujerumani inasaidia kufadhili mradi huo kwa kutoa dola milioni 2.7.

Soma pia: Baerbock afanya ziara Afrika Magharibi

Ivory Coast yenye wakazi milioni 30, ni nchi yenye uchumi mkubwa Afrika Magharibi hasa ukiilinganisha na mataifa ya eneo hilo yanayozungumza Kifaransa. Kama ilivyo kwa majirani zake wa Sahel ambao ni Ghana, Benin na Togo, nchi hiyo inakabiliwa pia na uasi wa makundi ya kigaidi kutoka Mali na Burkina Faso, ambako vikundi hivyo vimejiimarisha hasa katika maeneo ya mipakani.

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanwa kote ulimwenguni, kanda ya Sahel inachukuliwa kuwa eneo lililoathiriwa zaidi na ugaidi. Ziara hii ya siku mbili ya Baerbock inalenga kuthibisha kuwa serikali ya Ujerumani inadhamiria kuendelea kuwa na jukumu katika vita dhidi ya ugaidi huko Afrika Magharibi.

(Vyanzo: DPAE/AFP)