Baadhi ya shule zafungwa Mombasa kwa kukosa majengo imara
10 Oktoba 2019Shule hizo zifahamikazo kama APBET, zinatowa elimu katika mitaa ya kimasikini ya mabanda katika miji mikuu ya Mombasa, Nairobi, Kisumu na sehemu zilizo na ukame nchini Kenya. Mjini Mombasa kiasi cha shule 14 zimefungwa hivyo kutatiza masomo ya watahiniwa wasiopungua 36.
Moja ya shule zilizofungwa ni shule ya msingi ya Agatha iliyoko katika mtaa wa mabanda wa Bangladesh. Shule hiyo imefungwa kwa sababu ya kujengwa kwa mabati na kukosa miundombinu bora.
Kupitia kanuni ya mwaka 2009, serikali ya Kenya inazitambua shule hizo za kibinafsi za Mbadala ambazo aghalabu zimejengwa kwa mabati au mbao na kukosa miundombinu bora kulingana na kanuni za elimu, wizara ya elimu haikuzizingatia wakati ikitoa agizo la shule zisizokuwa na majengo bora kufungwa.
Wanafunzi wengi wasoma katika shule za majengo hatari
Amri hiyo ilitolewa na waziri wa elimu Dkt George Magoha kufuatia wanafunzi saba kufariki baada ya shule yao kuporomoka jijini Nairobi mwezi wa Septemba.
Katibu mkuu wa shule za mbadala za APBET nchini Kenya, Juma Athman Lubambo, anasema kutokana na uhaba wa shule za umma mijini, wanafunzi wengi wanasoma katika shule hizo.
Katika eneo bunge la Changamwe na Miritini mjini Mombasa kiasi cha shule 14 zimefungwa na katika kaunti ya Kwale shule 6.
Mtihani wa kitaifa wa darasa la nane utaanza mwishoni mwa mwezi huu na kwa sasa wizara ya elimu imewarundika wanafunzi hao katika shule za umma hadi pale shule hizo za APBET zitakapoboresha majengo yao.
Mwandishi: Faiz Musa