1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya uapisho Magufuli atarajiwa kutangaza mawaziri wapya

5 Novemba 2020

Baraza la mawaziri kufanya kazi zake za mwisho katika serikali ya Rais John Magufuli aliyeapishwa leo kuanza muhula wake mwingine wa pili na wa mwisho kwa mujibu wa katiba.

https://p.dw.com/p/3kuox
Tansania Amtseid des Präsidenten John Pombe Magufuli
Picha: Tanzania Presidential Press Service

Katika uhai wake wa miaka mitano, baraza hilo limeshuhudia likipitia mengi ikiwamo mawaziri wake kufutwa kazi na wengine kubadilishwa wizara.

Kuanzia Alhamisi hadi hapo litapotangazwa baraza lingine, shughuli zote zilizokuwa zikifanywa na mawaziri hao sasa zitafanywa na makatibu wakuu pamoja na wasaidizi wao.

Soma pia: Rais Magufuli aahidi kufanya kazi ya wapinzani

Kukoma kwa mawaziri hao katika majukumu yao ingawa kunawapa nafasi ya kupumua, lakini wakati huo huo pengine mapigo yao ya moyo yakaanza kuongeza kasi kwa hofu kwamba huenda wasirejee tena kwenye nyadhifa zao wakati Rais Magufuli atakapoliunda tena baraza lake jipya na kulitangaza.

Katika kipindi chake cha miaka mitano ikilinganishwa na mabaraza mengine ya mawaziri, baraza la mawaziri la Rais Magufuli linaongoza kwa kubadilishwa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo wale aliodai kuwatumbua kutokana na kushindwa kwenda na kasi yake.

Soma pia: Upinzani Tanzania wataka uchaguzi urudiwe

Baraza lake linamaliza muda wake likiwa na sura tofauti nne, kwanza wale walioingia kwenye nyadhifa zao na kuendelea kudumu mpaka wanamaliza ungwe ya kwanza ya miaka mitano, na kuna wale waliohamishwa kutoka wizara moja hadi nyingine.

Tatu kuna mawaziri waliong'olewa kwenye nafasi zao na baadaye kurejeshwa tena katika orodha ya baraza la mawaziri na mwisho wapo ambao walioondolewa kwenye nyadhifa zao na ikawa tiketi ya moja kwa moja na hawakurejea tena kwenye baraza hilo.

Waziri wa Mambo ya nje Tanzania PAlamagamba Kabudi
Waziri wa Mambo ya nje Tanzania PAlamagamba KabudiPicha: Getty Images/AFP/T.Karumba

Katika mchanganyiko huo pia kuna wanasiasa waliokuwa vyama vya upinzani walipewa nafasi katika baraza hilo mara walipovikahama vyama vyao na kujiunga CCM katika kile kilichofahamika wakati huo kuunga mkono juhudi.

Mabadiliko ya mara kwa mara ya Rais Magufuli katika baraza lake, yamekuwa yakielezwa kwa mitazamo mingi, lakini kwa mchambuzi huyu…… anaona kuwa.

Soma pia: Polisi Tanzania yawashikilia viongozi wa upinzani

Ingawa katika kipindi chote, Rais Magufuli alijipambanua kama kiongozi aliyetaka kuona mambo yakifanyika kwa haraka, lakini kama anavyosema Sam Ruhuza mwanasiasa wa siku nyingi na mchambuzi wa masuala ya siasa, sehemu kubwa ya mawaziri hao walishindwa kuwajibika moja kwa moja.

Kuapishwa kwa awamu nyingine kwa Rais Magufuli kunafungua milango kwa wanasiasa waliopenya kwenye majimbo yao kuingia katika serikali kama mawaziri na manaibu.

Ingawa ni mapema mno kubashiri ukubwa wa baraza lijalo na sura zipi zitajitokeza, lakini fumbo hilo huenda likapata mteguzi kwa kutupia macho vipaumbe ambavyo Rais Magufuli alivibainisha wakati wa kampeni zake.