1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Awamu ya pili ya uokozi yaanza Thailand

9 Julai 2018

Shughuli ya kuwaokoa vijana wa timu ya soka ya Thailand waliokwama kwenye pango kwa zaidi wa wiki mbili imeingia katika awamu ya pili. Tayari vijana wanne wamekwishaokolewa hadi sasa.

https://p.dw.com/p/31471
Thailand Rettungsaktion Tham Luang Höhle
Picha: picture-alliance/Xinhua/Chiang Rai PR office

Tayari vijana wanne wamekwishaokolewa hadi sasa, huku taarifa kutoka kwa baadhi ya maafisa zikielezea matarajio chanya ya shughuli hiyo ya uokozi ambayo kwa kipindi kirefu imekabiliwa na vikwazo, ambavyo ni pamoja na mvua kubwa iliyosababisha mafuriko. 

Kamanda wa kikosi cha uokozi, Narongsak Osottanakorn, amesema awamu ya pili ya uokozi imekwishaanza, na kuna matarajio makubwa ya vijana hao kuokolewa kwa vijana tisa waliokwama kwenye pango hilo, lililofurika maji hii leo. Alinukuliwa akisema anatarajia "habari njema muda mfupi ujao".

Aliwaambia waandishi wa habari mara tu baada ya kuanza kwa awamu hiyo ya pili ya shughuli hiyo ya uokozi kwamba, vifaa vyote viko tayari, ikiwa ni pamoja na mitungi ya hewa ya oksijini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia, Julie Bishop, ameelezea kuridhishwa na hatua iliyofikiwa hadi sasa, hususan baada ya vijana hao wanne kuokolewa. Australia imetuma wataalamu 19, ikiwa ni pamoja na daktari ambaye amekuwa akijihusisha zaidi na kuwapima wavulana hao, na kutoa kibali cha kuwaondoa kwa kuzingatia hali yao kiafya.

Thailand Höhle | Rettungsaktion Jugendliche
Vijana hao waliookolewa wanapatiwa matibabu, na familia zao bado hazijaanza kuwaona, hadi baada ya kuruhusiwa na madaktariPicha: Getty Images/L. DeCicca

Tayari vijana wanne wameokolewa hapo jana. Ingawa walikuwa na afya njema, lakini walikuwa na njaa kali. Maafisa wamesema, vijana hao hata hivyo, wametengwa na wazazi wao kwa sasa ili kuepusha hatari ya magonjwa ya kuambukiza. Amesema, madaktari ndio watakaokuwa wakitoa kibali kwa wazazi kuwaona, hadi hapo hatari hiyo itakapopungua.

Kamanda Narungsok, amewaambia waandishi wa habari kwamba, hali ya hewa hii leo ni nzuri na kiwango cha maji ni kidogo na hivyo waliamua kuanza mapema shughuli hiyo kuliko ilivyotarajiwa. Amesema, timu ni ileile iliyowaokoa vijana hapo jana jioni, lakini baadhi wamebadilishwa, kutokana na uchovu.

Lakini kwa upande mwingine kamanda huyo ameelezea wasiwasi kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa, baada ya mamlaka ya hali ya hewa kutangaza mvua kubwa itakayoonyesha kwenye eneo hilo mchana hii leo na kuendelea kwa wiki nzima, hatua inayoweza kusababisha ugumu kwenye zoezi hilo. 

Waziri wa mambo ya ndani wa Thailand, Anupong Paochinda aliwaambia waandishi wa habari hii leo kwamba vijana hao wanne waliookolewa jana, walikuwa wanaendelea vizuri. Familia zao zimearifiwa kujiandaa kuwatembelea hospitalini baada ya kupata matibabu, hii ikiwa ni kulingana na kituo cha televisheni cha eneo hilo, cha Thai PBS.

Mwandishi: Lilian Mtono/DPAE/APE/

Mhariri: Mohammed Khelef