1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asilimia 50 ya dawa Afrika Magharibi hazifai

1 Februari 2023

Hadi asilimia 50 ya dawa zilizopo Afrika Magharibi zinaripotiwa ama kuwa duni au ni bandia kwa mujibu wa tahadhari ya Umoja wa Mataifa kwenye ripoti yake kuhusu biashara ya magendo ya bidhaa za matibabu.

https://p.dw.com/p/4Mx3U
Symbolbild Mangel an Medizin an den Apotheken
Picha: Joly Victor/ABACA/picture alliance/dpa

Ripoti hiyo imeeleza zaidi kuwa bidhaa hizo huweza kusababisha hali ya mwili kupingana au kukataa dawa, sumu mwilini na vile vile huhujumu imani ya watu kwenye mifumo ya afya.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia dawa na magendo yake (UNODC) imesema kati ya Januari 2017 na Disemba 2021, bidhaa za matibabu zisizopungua tani 605, zilikamatwa Afrika Magharibi wakati wa operesheni ya kimataifa.

Ofisi hiyo imeongeza kuwa visa hivyo haviripotiwi mara kwa mara na huenda takwimu ziko juu zaidi.

Ripoti imesema kote kusini mwa Jangwa la Sahara, takriban dola milioni 44.7 hutumika kila mwaka kwa matibabu ya watu, ambao wametumia dawa bandia au ambazo viwango vyao vya ubora ni chini kutibu ugonjwa wa Malaria.

Takriban vifo 267,000 ambavyo huhusishwa na matumizi ya dawa hizo dhidi ya Malaria hutokea kila mwaka. Hayo ni kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO).