1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angola-Miaka mitano ya mkataba wa amani

Mohammed-Abdul-Rahman3 Aprili 2007

Pamoja na utajiri wake mkubwa bado wengi wanaishi katika umasikini

https://p.dw.com/p/CHlK
Usambazaji chakula wa Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP , 2006
Usambazaji chakula wa Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP , 2006Picha: WFP

Angola leo inatimiza miaka mitano tano ya amani baada ya miaka 27 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Taifa hilo linasherehekea siku hii ya kumalizika vita ikiwa moja wapo ya nchi zenye uchumi unaokua haraka barani Afrika, hali inayotokana zaidi na utajiri wa mafuta. Lakini utajiri huo bado haukusaidia kuinua maisha ya wakaazi wa taifa hilo.

Mkataba wa amani uliosainiwa kati ya serikali ya chama cha MPLA na waasi wa zamani UNITA Aprili 4 , 2002, ulimaliza mgogoro uliowauwa watu nusu milioni na kuharibu miundo mbinu ya nchi hiyo iliojinyakulia uhuru 1975 kutoka Ureno.

Wakati mikataba ya awali ilishindwa kuheshimiwa, mkataba huo wa mwisho kati ya pande hizo mbili umeweza kudumu, lakini pamoja na hayo kilichochelewa mpaka sasa ni uchaguzi. Hata hivyo baadhi ya wadadisi na wachambuzi wanaonya kwamba kushindwa kuhakikisha kwamba amani inawafaidisha watu wote, huenda likawa jambo linaloweza kuzusha matatizo na mtafaruku mwengine.

Tija inayotokana na mafuta imekua ni kubwa katika kipindi cha baada ya vita, kiasi ya kwamba Angola sasa ni nchi ya pili kwa ukubwa miongoni mwa zinazotoa mafuta barani Afrika , kusini mwa jangwa la Sahara baada ya Nigeria.

Kwa mujibu wa kampuni ya mafuta ya taifa SENANGOL, nchi hiyo itakua ikitoa mapipa milioni mbili kwa siku ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, ikilinganishwa na kiwango cha sasa cha mapipa milioni 1.4, wakati ambapo bei inazidi kupanda. Aidha faida imeshindwa kuwa tija kwa wanaoishi mashambani, ambako kiasi ya 70 asili mia ya wakaazi milioni 16 nchini humo wanapato la chini ya dola mbili kwa siku.

Tatizo jengine ni mabomu ya chini ya ardhi yalioachwa tangu wakati wa vita pamoja na miundo mbinu ilioharibiwa-yote hayo yakihujumu juhudi za kufufua kilimo. Wakati kilimo kilikua sekta kuu ya usafirishaji bidhaa n´gambo kabla ya uhuru, kilikua katika nafasi ya 8.6 tu asili mia ya pato jumla la taifa mwaka 2006, wakaazi mafuta sasa ni 57 asili mia.

Maaskofu nchini Angola walikusanyika mwaka jana kuzungumzia kiwango cha umasikini, wakijiuliza inakuaje Angola yenye utajiri mkubwa wa mafuta na madini ya almasi na ardhi yenye rutuba, inatajwa kuwa ni miongoni mwa nchi masikini duniani ?

Rais Jose Eduardo dos Santos aliye madarakani tangu 1979 baada ya kifo cha Rais wa kwanza Agostinho Neto, alikua aitishe uchaguzi mwaka jana, lakini ratiba ikacheleweshwa na sasa uchaguzi wa bunge umepangwa mwaka ujao na ule wa Rais 2009.

Wakati Angola leo ikisherehekea miaka mitano ya mkataba wa amani, nini matumaini ya Waangola ? Rafael Marques mwanaharakati wa haki za binaadamu nchini humo anasema,“ Ni uwezo wao wa kusamehe kwa maumivu waliyoyapata wakati wa vita na chuki ambayo kwa muda mrefu ndiyo ilioongoza maisha yao. Wengi wameyaweka hayo nyuma.Ni suala la kusonga mbele katika ujenzi awa jamii mpya.Bado kuna ishara za ukosefu wa kuvumiliana lakini hayo yanatoka upande wa chama tarala MPLA. Changa moto kubwa leo ni jinsi ya kujenaga jamii mpya bila ya mdahalo. Hakuna mdahalo kati ya umma na serikali.”