1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Afrika Magharibi iongeze vita dhidi ya rushwa

11 Julai 2023

Shirika la Kimataifa la Amnesty International limesema mataifa ya Afrika Magharibi na Kati lazima yafanye juhudi kubwa katika vita dhidi ya ufisadi na kuwacha kuwatesa watetezi wa haki za binaadamu wanaofichua uovu huo

https://p.dw.com/p/4TiX7
Kamerun | Trauer um Martinez Zogo
Picha: Daniel Beloumou Olomo/AFP/Getty Images

Katika ripoti iliyotolewa leo katika Siku ya Kupambana na Rushwa Afrika, shirika la Amnesty International limelaani matukio ya kukamatwa, kuteswa, kuzuiliwa, na kutozwa faini kubwa na hata kuuliwa kwa wanaharakati wa haki za binaadamu wanaopigana na rushwa katika nchi 19 za Afrika Magharibi na Kati.

Katibu Mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard anasema watu hao wana jukumu muhimu katika kupambana na rushwa na hivyo kutetea haki za binaadamu. Hata hivyo mara kwa mara wanakumbwa na mashambulizi, vitisho, unyanyasaji, na mateso kwa kufichua ukweli.

Interview mit Agnès Callamard | Menschenrechte in Taiwan
Agnes Callamard, mkuu wa Amnesty InternationalPicha: Amnesty International Taiwan

Shirika hilo la haki za binaadamu limetaja mfano wa mwandishi Habari wa Cameroon Martinez Zogo, ambaye limesema alikuwa anachunguza tuhuma za ubadhirifu wa mamia ya mabilioni ya faranga za Afrika Magharibi na Afrika ya Kati na watu walio karibu na serikali.

Zogo alitekwa nyara na watu wasiojulikana mnamo Januari 17, na mwili wake ukapatikana baadae ukiwa umekatwa vikungo vyake katika eneo moja nje ya mji mkuu Yaounde.

Nchini Togo, mwandishi Habari Ferdinand Ayite alikamatwa mnamo Desemba 10, 2021, baada ya kuwatuhumu maafisa wawili wa serikali kwa rushwa.

Alihukumiwa mnamo Machi 15, Pamoja na mwenzake, kifungo cha miaka mitatu jela na kutozwa faini ya faranga milioni 3 karibu na dola 5,000 kwa kile kilichotajwa kuwa ni "kudharau mamlaka” na "kueneza propaganda.”

Amnesty imesema Ayite na mwenzake walikata rufaa dhidi ya uamuzi huo lakini mwishowe wakalazimika kukimbia nchi wakihofia usalama wao.

Uozo ulofichika katika demokrasia imara ya Ghana

Nchini Niger, mwandishi Habari na mwanablogu Samira Sabou alitiwa hatiani Januari 2022 kwa makosa ya kuchafua sifa kwa kutumia mawasiliano ya kielektroniki, chini ya sheria ya nchi hiyo ya uhalifu wa mitandaoni. Alipewa kifungo cha mwezi mmoja jela na faini ya dola 100.

Waendesha mshitaka walitaja uamuzi wake wa kuchapisha upya Makala ya Mei 2021 kutoka shirika lenye makao yake mjini Geneva la Global Initiative against Transnational Organized Crime, ambayo ilidai kuwa shehena ya dawa za kulevya iliyokamatwa na shirika la kupambana na biashara haramu nchini Niger ilinunuliwa tena na walanguzi wa dawa za kulevya na kurejeshwa kisiri sokoni.

Callamard ametoa wito kwa serikali za eneo hilo kuushughulikia utamaduni ulioenea wa kutokujali sheria ambao unaendelea kuchochea ufisadi uliokithiri..na kuwanyima wawathiriwa fursa ya kupata haki.

Amnesty International imeyataka mataifa ya Afrika Magharibi na Kati kupitisha sheria, sera na taratibu ambazo zinalinda kikamilifu dhidi ya ufisadi.

Kwa sasa ni Cote d'Ivoire, Mali na Niger pekee ambazo zimepitisha sheria zinazowalinda watetezi wa haki za binaadamu, na ni Ghana pekee ambayo ina sheria maalum inayowalinda wafichua rushwa.

AFP