1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AKK: Merkel yuko salama, kwa sasa

9 Desemba 2018

Katika mahojiano na DW, Annegret Kramp-Karrebauer, kiongozi mpya wa chama cha Christian Democratic Union - CDU amesema anataka Angela Merkel akamilishe muhula wake wa Ukansela

https://p.dw.com/p/39klg
Germany Merkel's Party Annegret Kramp-Karrenbauer Angela Merkel
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Kiongozi mpya wa chama cha Christian Democratic Union – CDU nchini Ujerumani Annegret Kramp-Karrenbauer alizungumza na DW muda mfupi baada ya kukamilika mkutano wa chama hicho. DW ilimuuliza kama bado anafikiri kuwa Merkel atasalia madarakani kwa miaka mitatu iliyobaki ya muhula wake.

Kuhusu kuwa Kansela: Kramp-Karrenbauer alisema: "Tuna serikali kuu ambayo imechaguliwa kwa kipindi hiki. Angela Merkel amesema yupo kukamilisha muhula wa bunge la sasa. Na mkutano wa chama umeonyesha wazi kuwa hicho ndicho wanachama wanakitamani – na ndio matamanio yangu ya kibinafsi pia. "Na pia naliona kuwa jukumu langu kama kiongozi wa chama tawala kuhakikisha kuwa serikali hii ina utulivu inaouhitaji ili kutimiza ahadi ilizotoa kwa wapiga kura.”

Deutschland CDU-Parteitag in Hamburg Friedrich Merz
Friedrich Merz alionekana kusikitishwa na matokeoPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

AfD: 

Mwaka ujao, chaguzi kadhaa za majimbo zitafanyika mashariki mwa Ujerumani. Chama cha siasa kali za kizalendo AfD kimekuwa na mafanikio hasa upande wa mashariki.  DW iliuliza, "Ni vipi unatumai kuwarejesha wapiga kura hawa?” "Kwa nguvu zetu wenyewe,” Alijibu Kramp-Karrenbauer. "Kwanza, hatutafuata kile ambacho vyama vingine vinafanya, hata kama kampeni hizi za uchaguzi wa majimbo hazitakuwa rahisi. Badala yake tunataka kujenga nguvu zetu katika maeneo hayo kama CDU. "Kuna mada nyingi za kikanda, maeneo mengi tunayofanya vyema. Katika majimbo ambayo sisi ni wapinzani, kuna ukosoaji ulio sahihi kuelekea wale wanaotawala.  Kutakuwa bila shaka na mada zaidi za jumla – kama vile masuala ya kijamii na pensheni. Tutapaswa kujipanga vyema. Lakini kama nilivyosema, lengo letu ni kuwashawishi watu na sio kujishawishi sisi.

Ushindi mwembamba: Kramp-Karrenbauer alipata asilimia 51 tu katika duru ya pili ya uchaguzi wa chama dhidi ya mpinzani wake mkuu, mfanyabiashara na mhafidhina wa tangu jadi Friedrich Merz. Mgombea wa tatu, Jens Spahn aliondolewa katika duru ya kwanza. Wengi katika chama chake wangependelea chama cha CDU kiwe cha kihafidhina zaidi ili kupambana na wapinzani wa siasa kali za kizalendo. DW ilimuuliza nini ananchopanga kuwafanyia wale wanaohisi kukata tamaa. "Mkutano wa chama umegawanywa kwa kiwango cha mtu binafsi. Lakini ilikuwa wazi kabla ya hapo kuwa wagombea pia walikuwa na maoni sawa," Kramp-Karrenbauer aliiambia DW. "Kwa mfano, kama Friedriech Merz na Jens Spahn, naamini taifa linapaswa kutekeleza utawala wa sheria. Nilijifunza hilo wakati nilipokuwa waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Saarland. Na ni kitu ambacho tunataka tuanzishe katika mazungumzo kuhusu uhamiaji na usalama wa ndani mwaka ujao."

Deutschland CDU-Parteitag in Hamburg Jens Spahn
Jens Spahn hakupewa nafasi kubwaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Maandamano Ufaransa: Watu wanapambana dhidi ya ukosefu wa usawa wa kijamii nchini Ufaransa. Unaweza kujifunza chochote kuhusu hilo nchini Ujerumani? "Nadhani Ujerumani ipo katika hali tofauti, kwa sababu kupitia uchumi wa soko la kijamii na mfumo wetu wa ushirikiano wa kijamii, tuna mfumo ambao masuala mengi na migogoro vinajadiliwa kila mara na kutatuliwa katika miundo ya utaratibu. Na natumaini kabisa kwamba sisi Ujerumani tunaweza kuwa na amani, amani ya kijamii ambayo tunayo kwa sababu ya hilo. "Kwa sababu iwe ni Ufaransa au katika mataifa mengine – unaweza kuona jinsi ni tatizo kubwa wakati sheria zilizokubaliwa zinapovunjwa na wakati mizozo – hata wakati inapokuwa ya haki – inapogeuka kuwa vurugu."

Kramp-Karrenbauer ni nani? 

Annegret Kramp-Karrenbauer alishinda kinyang'nyiro cha kumrithi Merkel baada ya miaka 18 ya kuwa katika uongozi wa CDU. AKK – kama anavyofahamika kwa ufupi – alihudumu kama waziri wa mambo ya ndani na waziri kiongozi wa jimbo la kusini magharibi la Saarland. Aliongoza serikali ya muungano wa CDU-SPD katika jimbo hilo kabla ya kujiuzulu na kuwa katibu mkuu wa CDU. Anazingatiwa kuwa mwanasiasa wa siasa za wastani ambaye anaweza kuendeleza siasa za wastani za Merkel.

Nini kipaumbele chake? 

Kama kiongozi wa chama, kazi ya kwanza kwa AKK ni kukiunganisha chama kilichogawika cha CDU, na kulisaidia jahazi la serikali ya muungano na chama cha siasa za wastani za mrengo wa kulia cha SPD. Muungano huo umekaribia kusambaratika mara kadhaa tangu ulipoundwa mwezi Machi.

Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Iddi Ssessanga

https://bit.ly/2G8fHn1