1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Katika Magazeti ya Ujerumai ,Boko Haram waendelea kuua watu

Abdu Said Mtullya22 Juni 2012

Wiki hii magazeti Ujerumani yameandika juu ya matukio ya kaskazini mwa Afrika,ambako jeshi la Misri linajaribu kuzuia juhudi za kuleta demokrasia. Pia yameandika juu ya Nigeria.

https://p.dw.com/p/15Jet
Wanajeshi wa Nigeria pia wanashambuliwa na Boko Haram
Wanajeshi wa Nigeria pia wanashambuliwa na Boko HaramPicha: dapd

Gazeti la "Mittelbayerische"limetoa maoni juu ya matukio ya nchini Misri kwa kusema: Wakati wabunge wa Ujerumani wanalumbana juu ya hatua ya nchi yao ya kuiuzia vifaru Saudi Arabia, Waziri wa mambo ya nje Guido Westerwelle ametoa ujumbe kwa mtu atakaechaguliwa kuwa Rais wa Misri.Katika ujumbe huo Waziri Westerwelle ametoa mwito wa kufuata misingi ya demokrasia.

Lakini mhariri wa gazeti la "Mittelbayerische" anasema ni dhihaka iliyoje kwa Waziri Westerwelle kutoa mwito huo wakati Marekani ambae ni mfadhili mkuu wa jeshi la Misri inasema kuwa ni bora kuwa na utawala wa kidikteta unaoaminika kuliko kuwa na demokrasia dhaifu. Gazeti la "Mittelbayerische" linasema kwa baadhi ya wanamikakati ya kisiasa, hiyo ni hali halisi ya nchini Misri, lakini kwa watu wa Misri mtazamo huo wa Marekani ni usaliti.

Gazeti la "Berliner Zeitung" pia limeandika juu ya matukio ya nchini Misri.Linasema katika makala yake kwamba hakuna kitakachofanyika nchini Misri bila ya majenerali .Gazeti hilo limemkariri Jenerali Mamdouh Shahin akiwaambia waandishi wa habari kwamba mamlaka ya uongozi wa nchi lazima yagawanywe na madhali Bunge limevunjwa jeshi ndilo litakalochukua mahala pa Bunge.

Kundi la waislamu wenye itikadi kali Boko Haram limeendelea kufanya mashambulio karibu kila siku nchini Nigeria. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linayaita mashambulio hayo kuwa ni hatua zinachokuliwa na masikini wa Nigeria kulipiza kisasi. Mwandishi wa gazeti hilo Jochen Stahnke ameripoti:

"Ghasia kaskazini mwa Nigeria zinatishia kwenda mrama kiasi cha kutoweza kudhibitika.Kundi la waislamu wenye itikadi kali,Boko Haram linafanya mashambulio takriban kila siku.Vijana wa kikristo na wa kiislamu wanachinjana.Sasa pana wasi wasi mkubwa wa kutokea vita vya kidini nchini Nigeria.Lakini chanzo chake hasa siyo cha kidini.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linatilia maanani katika makala yake kuwa vijana wasiokuwa na ajira wanaandikishwa kwa urahisi na makundi ya kigaidi. Gazeti hilo linasema vijana hao wanakasirishwa na vitendo vya rushwa vinavyofanywa serikalini. Kwani wanatambua kwamba, licha ya utajiri mkubwa wa mafuta nchini Nigeria, vijana hao wanaendelea kuishi katika umasikini mkubwa.

Gazeti la "die tageszeitung" pia limeandika juu ya matukio ya nchini Nigeria kwa kutilia maanani kwamba watu zaidi ya 80 wameuawa katika siku za hivi karibuni kutokana na mapambano baina ya vijana wa kiislamu na wa kikristo.

Hata hivyo gazeti la "Handelsblatt" linatukumbusha kwamba kila kapa inazo pande mbili,za usubi na uroda.

Gazeti hilo linapusha habari juu ya upande wa uroda nchini Nigeria.Limeandika taarifa juu ya mfanyabiashara anaeitwa Aliko Dangote.Jee Dangote ni nani ? Gazeti la "Handelsblatt" linatufahamisha Mfanyabiashara huyo ambae ni Bilionea anadhamiria kuingia katika soko la hisa la London.Utajiri wake unakadiriwa kufikia dola bilioni 12. Lakini hautokani na biashara ya mafuta, bali na biashara ya saruji. Alianza kupata mafanikio mwishoni mwa miaka ya 70 baada ya kupewa leseni ya kuagiza,sukari,mchele na saruji.Na sasa ameuamua kuingia katika soko la hisa la London kuanzia mwaka ujao.

Gazeti la "die tageszeitung" linatahadharisha juu ya hatari ya kutoweka kwa ndovu barani Afrika kutokana na biashara haramu ya vipusa. Gazeti hilo linaarifu katika makala yake kwamba kutokana na uroho wa wachina wa pembe za ndovu, wanyama hao wamo hatarini kupungua na hata kutoweka barani Afrika kama walivyotoeka China kwenyewe.

Gazeti hilo limelinukuu shirika la ulinzi wa wanyama pori duniani WWF likisema kuwa idadi ya tembo waliuliwa kutokana na biashara ya vipusa imeongezeka sana katika muda wa miaka mitatu iliyopita barani afrika.Kwa mujibu wa shirika la ulinzi wa wanyama pori, bei ya pembe za ndovu imeongezeka nchini China kutoka Euro 100 kwa kilo mnamo mwaka 2002 hadi kufikia Euro 1900 kwa kilo mwaka jana.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Othman Miraji