Afrika inahitaji kuendeleza mpango wa usafirishaji nafaka
16 Juni 2023Mataifa makuu ya Afrika yamesisitiza haja ya uagizaji wa nafaka kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa chakula, wakati rais wa Urusi Vladmir Putin akijiandaa kujadili na viongozi wa bara hilo hatma ya makubaliano yanayoruhusu usafirishaji salama wa chakula na mbolea kutoka Ukraine kupitia Bahari Nyeusi.
Putin amesema jana kuwa Urusi ilikuwa inazingatia kujitoa kwenye mpango huo ulioratibiwa na Umoja wa Mataifa na Uturuki Julai mwaka jana, kwa sababu usafirishaji wa nafaka zake na mbolea vinaendelea kukumbana na vizingiti. Mpango wa sasa wa usafirishaji nafaka utamalizika muda wake Julai 17.
Ujumbe wa viongozi wa Kiafrikaunatarajiwa kuzitembelea Ukraine na Urusi kuanzia mwishoni mwa wiki hii, katika juhudi ka kumaliza vita vya miezi 16 vya Urusi. Putin amesema anapanga kutumia nafasi hiyo kuibua suala hilo.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, anaamini Putin na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy wanakubaliana naye juu ya umuhimu wa usafirishaji wa nafaka kwenda Afrika, kwa ajili ya kupunguza ukosefu wa chakula, kwa mujibu wa msemaji wa Ramaphosa, Vincent Magyenya.