1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON 2019: Mauritania yakaribishwa kwa kuchapwa 4-1 na Mali

Daniel Gakuba
25 Juni 2019

Katika michuano ya Afcon 2019 inayoendelea Misri, jana Ivory Coast ilishinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Afrika Kusini katika kundi gumu la D. Jumanne ni Ghana dhidi ya Benin na Cameroon ikizipiga na Guinea-Bissau.

https://p.dw.com/p/3L312
Fußball Africa Cup of Nations 2019 | Mali vs  Mauretanien
Picha: Getty Images/AFP/F. Senna

   Ushindi mnono zaidi katika mechi za Jumatatu (24.06.2019) uliiendea timu ya taifa ya Mali, ambayo iliikaribisha Mauritania inayoshiriki kwa mara ya kwanza katika michuano hii, kwa kuifungashia furushi la magoli 4 kwa 1 la kufutia machozi. Kwa ushindi huo Mali imekaa kileleni katika kundi E linalozijumuisha Angola na Tunisia, ambazo zilitoka sare.

Soma zaidi:  Kenya na Tanzania zaangukia pua

Mauritania ilikuwa timu ya tatu kushuka uwanjani kwa mara ya kwanza katika mashindano haya, na ndio imesuasua ikilinganishwa na nyingine mbili, Burundi ambayo iliipa taabu Nigeria licha ya kupoteza mechi yao kwa goli 1-0, na Madagascar iliyojikakamua na kutoka sare ya magoli 2-2 dhidi ya Guinea.

Angola yatibua furaha ya Tunisia

Fußball Africa Cup of Nations 2019 Elfenbeiküste - Südafrika
Jonathan Kodjia wa Ivory Coast akimponyoka Bhule Mkhwanazi wa Afrika KusiniPicha: Reuters/M. A. El Ghany

Mechi nyingine katika kundi hili la E ilikuwa baina ya Tunisia na Angola. Ingawa Tunisia ilifunga goli la kuongoza mnamo kipindi cha kwanza kupitia mkwaju wa penalty, baada ya Dani Massungona kujitandaza na kumbwaga chini Naim Sliti katika eneo la hatari.

Angola ilisawazisha katika ngwe ya pili kufuatia kosa la mlinda lango wa Tunisia, Farouk Ben Mustafa, ambaye aliutema mpira na kuudondosha kwenye miguu ya Djalma Campos wa Angola, ambaye aliitumia vizuri hisani hiyo na kuingiza bao laini katika lango lililoachwa wazi. 

Zaidi kuhusu Afcon 2019: Michuano ya AFCON yafungua pazia nchini Misri 

Mbali na mechi za kundi E, Jumatatu pia zilichezwa mechi kati ya Ivory Coast na Afrika Kusini kutoka kundi D. Goli pekee la Ivory Coast lililomiminwa kimiani na Jonathan Kodjia, kwa kuunganisha krosi safi kutoka kwa Max Gradel, lilitosha kuisukuma hadi nafasi ya kwanza katika kundi la D, linalotazamwa kama kundi la kifo katika Afcon ya mwaka huu, likiwa na timu tatu ambazo ziliwahi kutwaa kombe la mashindano hayo. Timu hizo ni Ivory Coast yenyewe, Afrika Kusini na Morocco.

Kikosi cha nyota wa kimataifa

Ivory Coast ilishuka na majina makubwa katika uwanja wa soka, kama Wilfried Zaha wa Crystal Palace, Serge Aurier wa Tottenham, Jean Michael Seri wa Fulham na Max-Alain Gradel wa Toulouse, na muda wote ilionekana kitisho mbele ya Bafana Bafana ya Afrika Kusini.

Uhondo jioni ya Jumanne ni baina ya Cameroon, bingwa wa sasa  ambayo ilipokonywa fursa ya kuyaandaa mashindano ya mwaka huu, na Guinea Bissau, nayo Ghana itacheza mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Benin.

ape, rtre