1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA : Mkuu wa Umoja wa Afrika kuzuru Ufaransa

17 Oktoba 2005
https://p.dw.com/p/CEQy

Rais wa tume ya Umoja wa Afrika ataitembelea Ufaransa wiki hii kujadili ushirikiano juu ya masuala ya amani na usalama kati ya Umoja wa Afrika na Ufaransa,uhamiaji na msaada wa maendeleo kwa bara hilo.

Rais wa zamani wa Mali Alpha Omar Konare atakuwa anafanya ziara yake ya kwanza rasmi nchini Ufaransa wakati atakapoondoka katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Abba Ijumaa wiki hii kwa mazungumzo ambayo yanatazamiwa kulenga mchakato wa amani ulioko mashakani nchini Ivory Coast na wahamiaji wa Afrika wanaokimbilia Ulaya.

Ziara hiyo ya Konare nchini Ufaransa ambayo itamalizika tarehe 27 mwezi wa Oktoba inakuja huku hali ya kukosa utulivu ikiendelea nchini Ivory Coast pamoja na mzozano wa kisiasa katika koloni hilo la zamani la Ufaransa ambapo uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika mwisho wa mwezi umefutwa.

Ziara hiyo ya Konare pia inafanyika wakati suala tete la wahamiaji wa Afrika wanaokimbilia Ulaya limefikia kipeo chake likimbatana na vifo vya wahamiaji katika miezi ya hivi karibuni wakijaribu kuingia kwenye maeneo ya Uhispania yalioko kwenye ardhi ya Mororoco.

.