1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yaunga mkono uchunguzi wa kimataifa wa ajali ya ndege

Lilian Mtono
25 Januari 2024

Ikulu ya Kremlin imesema inakubaliana na ombi la Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine la kutaka uchunguzi wa kimataifa wa ajali mbaya ya ndege ya kijeshi ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4bg34
Ukraine | Vita | Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky
Rais Volodymyr Zelensky amesema kuna umuhimu wa taasisi za kimataifa kuchunguza zaidi eneo la ajali ya ndege ya kijeshi ya Urusi na kusababisha vifo vya watu 74Picha: Presidential Office of Ukraine/SvenSimon/picture alliance

Zelensky alitoa mwito wa uchunguzi siku moja baada ya kisa hicho. Huku mengi yakiendelea kujitokeza kuhusiana na ajali hiyo, mchana huu Ukraine imekana kupokea ombi la mdomo ama maandishi kutoka kwa Urusi la kuweka usalama kwenye eneo la anga ambako ndege hiyo ilianguka. 

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema "kama Zelensky anamaanisha uchunguzi wa kimataifa juu ya uhalifu wa utawala wa Kyiv, basi ni dhahiri kwamba upo umuhimu mkubwa wa kitendawili hicho kuteguliwa."

Peskov aidha amerudia madai Wizara ya Ulinzi ya Urusi kwamba Ukraine iliidungua ndege hiyo ya usafirishaji ya kijeshi jana Jumatano, katika jiji la Belgorod nchini Urusi. Moscow imesema wanajeshi 65 wa Ukraine ni miongoni wa abiria 74 waliokufa baada ya ndege hiyo kushambuliwa.

Soma pia: Ukraine yataka uchunguzi wa kimataifa katika ajali ya ndege ya Urusi

"Wafungwa wa kivita wa Ukraine walikuwa wakisafirishwa kwenda Belgorod kwa ajili ya kubadilishana wafungwa kufuatia makubaliano kati ya Moscow na Kyiv. Lakini tofauti na hayo, upande wa Ukraine ulifyatua kombora kutokea jimbo la Kharkiv," alisema Peskov. 

Baraza la Usalama la UN lakutana kuijadili Ukraine | Volodymyr Zelensky
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linakutana kwa dharura kujadilia ajali ya ndege ya Urusi, kufuatia ombi la UrusiPicha: Spencer Platt/Getty Images/AFP

Wizara ya Ulinzi ya Urusi, ikiangazia taarifa za rada yake imesema vikosi vya Ukraine viliidungua ndege hiyo kwa kutumia mfumo wa kuzuia makombora angani uliopo katika jimbo la Kharkiv. Lakini hadi sasa Ukraine haijathibitisha madai kwamba makombora yake ndiyo yaliidungua ndege hiyo ama hata ikiwa wanajeshi wake walikuwemo ndani ya ndege hiyo, ingawa awali ilikiri kwamba Urusi inashughulikia hatua hiyo ya kubadilishana wafungwa.

Urusi yasema iliiarifu Ukraine juu ya mabadilishano hayo.

Urusi inasisitiza kwamba Kyiv iliarifiwa juu ya muda na namna ambavyo wafungwa hao wa Ukraine watakavyosafirishwa ili kujipanga mapema. Peskov hakueleza ikiwa kuna mpango mwingine wa kubadilishana wafungwa siku za usoni.

Lakini hata hivyo, Kamishna wa Haki za binaadamu nchini Ukraine Dymitro Lubinets amesema Kyiv hadi sasa haiijapata ushahidi wowote kuwa ndege hiyo ilikuwa imewabeba wafungwa hao wa kivita.

Kiza bado ni kinene juu ya ajali hiyo yakiwa yamepita masaa 24 sasa tangu ilipotokea. Wachambuzi kutoka Taasisi ya Masomo ya Vita ya nchini Marekani, ISW iliyopo mjini Washington wamesema si rahisi kuyathibitisha madai ya Urusi ama ya Ukraine. Imesema Urusi inataka kutumia kisa hicho kupandikiza chuki ya watu dhidi ya serikali yao, lakini pia kudhofisha zaidi ushirika wa Ukraine na mataifa ya magharibi kwa kuibua madai yasiyothibitishwa.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana leo kuijadili ajali hiyo. Ufaransa ambayo ndiyo rais wa sasa wa Baraza hilo la usalama, imesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov ndiye aliomba kufanyika kwa kikao hicho cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuijadili ajali hiyo, ambayo ameiita ''shambulizi la kigaidi.''