1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Ukraine yataka uchunguzi wa kimataifa ajali ya ndege Urusi

Grace Kabogo
25 Januari 2024

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametaka uchunguzi wa kimataifa ufanyike kuhusu ajali ya ndege ya jeshi la Urusi iliyotokea Jumatano kwenye jimbo la Belgorod.

https://p.dw.com/p/4bedU
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine, Volodymyr ZelenskyPicha: AFP/Getty Images

Akizungumza Jumatano usiku, Zelensky amesema idara ya ujasusi ya kijeshi ya Ukraine, HUR inajaribu kuchunguza zaidi kuhusu hatma ya wafungwa kadhaa wa kivita wa Ukraine ambao walikuwamo ndani ya ndege hiyo.

''Idara ya usalama ya Ukraine inachunguza kwa kuzingatia mazingira yote. Nimemuagiza waziri wa mambo ya nje kuwajulisha washirika wetu kuhusu taarifa zote zilizopo. Nchi yetu inasisitiza kufanyika kwa uchunguzi wa kimataifa,'' alisisitiza Zelensky.

Zelensky amesema ni wazi kuwa Urusi inacheza na maisha ya wafungwa wa Ukraine, pamoja na hisia za jamaa zao, na hisia za jamii ya Ukraine. Gavana wa Belgorod, Vyacheslav Gladkov amesema abiria wote 74 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wamekufa. Gladkov amesema taarifa hizo zimethibitishwa na vyombo vya habari vya Urusi.

Visanduku vya kuhifadhia data za safari za ndege vyapatikana 

Eneo la Belgorod ambalo ndege ya kijeshi ya Urusi ilianguka Jumatano
Eneo la Belgorod ambalo ndege ya kijeshi ya Urusi ilianguka JumatanoPicha: UGC/AP/picture alliance

Shirika la habari la serikali ya Urusi, RIA liliripoti kuwa ndani ya ndege hiyo ya kijeshi aina ya Ilyushin chapa II-76, walikuwemo wafungwa wa kivita 65 wa Ukraine waliokuwa wakisafirishwa kwenda Belgorod kwa ajili ya mpango wa kubadilishana wafungwa, wafanyakazi sita wa ndege hiyo, pamoja na wasindikizaji watatu.

Wakati huo huo, RIA, imesema visanduku vya kuhifadhia data za safari za ndege kutoka kwenye ndege hiyo ya kijeshi ya Urusi iliyoanguka jana Belgorod, vimepatikana na vimehifadhiwa. Urusi imeishutumu Ukraine kwa kuidungua ndege hiyo. Hata hivyo, Ukraine haijazungumza chochote kuhusu madai hayo ya Urusi.

Huku hayo yakijiri, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana Alhamisi kuijadili ajali hiyo ya ndege ya kijeshi ya Urusi. Ufaransa ambayo ndiyo rais wa sasa wa Baraza hilo la usalama, imesema kuwa Urusi ndiyo imeomba mkutano huo ufanyike.

Urusi yataka ajali ijadiliwe Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov Picha: Alexander Shcherbak/Tass/IMAGO

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov aliomba kufanyika kwa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuijadili ajali hiyo, ambayo ameiita kama ''shambulizi la kigaidi.''

Soma zaidi: Urusi na Ukraine zabadilishana wafungwa

Ama kwa upande mwingine, mbunge wa Urusi na mjumbe wa kamati ya ulinzi ya bunge, Andrei Kartapolov, amesema Alhamisi kuwa Urusi na Ukraine zitaendelea na mpango wa kubadilishana wafungwa wa kivita, licha ya kudunguliwa kwa ndege hiyo. Shirika la habari la Interfax limemnukuu Kartapolov akisema kuwa Urusi itazungumza hata na ''shetani na adui'' ili kuwarejesha wanajeshi wake waliotekwa.

Katika hatua nyingine, Kikosi cha Anga cha Ukraine kimesema mfumo wake wa ulinzi wa anga umezidungua droni 11 kati ya 14 zilizorushwa katika shambulizi lililofanywa na Urusi, usiku wa kuamkia Alhamisi kwenye mikoa ya Odesa na Mykolaiv, kusini mwa Ukraine. Gavana wa Odesa, Oleh Kiper amesema watu wawili wamejeruhiwa katika shambulizi la Odesa.

(AFP, DPA, Reuters)