1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwenyekiti wazamani wa CENI azindua chama cha kisiasa Congo

Amina Mjahid
27 Februari 2023

Mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Corneille Nangaa alizindua chama chake cha kisiasa, miezi kadhaa kabla ya uchaguzi unaotarajiwa mwezi Disemba.

https://p.dw.com/p/4O190
Demokratischen Republik Kongo | Wahlkommision |  Corneille Nangaa
Picha: DW/F. Quenum

Baada ya kuzinduliwa chama chake kipya cha  ADCP, Corneille Nangaa sasa amejitosa rasmi kwenye ulingo wa siasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alieleza kwamba nchi hii imeshindwa kuwapa Wakongo usalama katika nyanja zote na hivyo, Nangaa akahimiza kuhusu kazi na uzalendo akisema ndivyo vinapaswa kuwa mtindo wa maisha hapa Kongo. 

"Sisi kwenye ADCP tumewasilisha toleo letu la kweli la kisiasa. Yaani, kuwafundisha watoto tangu shule ya chekechea jinsi ya kupenda nchi hii. Tunapaswa kuwa na unyenyekevu wa mwanzo dhaifu. Kawaida, kila nchi huendelea kupitia biashara na kwa hivyo biashara lazima ziundwe. Tunahitaji ujasiriamali," alisema Nangaa.

Upinzani wakosoa zoezi la usajili wa wapigakura nchini Congo

Corneille Nangaa ambaye aliiongoza tume ya taifa ya uchaguzi CENI tangu mwaka 2015 hadi 2021 alieleza kuwa ADCP itakuwa na wagombea kwenye ngazi zote katika uchaguzi wa Decemba. Lakini alisisitiza kuwa mazingira ya sasa bado hayajatoa uhakika wa kufanyika uchaguzi bora.

Upinzani wataka Nangaa akamatwe

Martin Fayulu
Kiongozi wa upinzani Congo Martin Fayulu Picha: Nicolas Maeterlinck/BELGA/picture alliance

Awali aliliambia jarida la Jeune Afrique kwamba makubaliano ya kisiasa yaliyofikiwa kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2018 yameiokoa nchi hii kutokana na umwagaji damu. Lakini muungano wa upinzani wa Lamuka unaamini kuwa Corneille Nangaa alitengeneza matokeo. Muungano huo unataka Nangaa akamatwe mara moja.

Tshisekedi athibitisha uchaguzi utafanyika 2023 nchini Congo

"Corneille Nangaa anapashwa kueleza jinsi alivyokubali kukiuka Katiba kwa kutupilia mbali matokeo halisi ya uchaguzi wa urais ili kutangaza matokeo ya makubaliano ya kisiasa. Kwa jina la wakongo, hakimu amuulize ni nani aliyeandaa mauaji ya wakongo ili kuwe na umwagaji damu. Lamuka inatoa masaa 48," alisema , Prince Epenge, mmoja wa wasemaji wa Lamuka.

Ukimbizi shida DRC

Ni matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2018 yaliomfanya Félix Tshisekedi rais wa Kongo. Jambo ambalo lilitupiliwa na wachunguzi kadhaa wakiwemo Kanisa Katoliki na Umoja wa Afrika waliosisitiza kuwa mshindi wa kweli hakutangazwa.

Na tangu hapo Martin Fayulu bado anaendelea kujitaja kuwa rais mteule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Mwandishi: Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.