1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani wakosoa zoezi la usajili wa wapigakura nchini Congo

Mithima de la Chance27 Desemba 2022

Wapinzani Martin Fayulu, Augustin Matata Ponyo na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel mnamo mwaka 2018 Daktari Denis Mukwege wanakosoa namna ambavyo tume ya uchaguzi CENI inavyoendesha shughuli za kuwasajili wapigakura.

https://p.dw.com/p/4LRxy
Wapinzani Martin Fayulu (kushoto) na Matata Ponyo wataka uchaguzi bora nchini Kongo
Wapinzani Martin Fayulu (kushoto) na Matata Ponyo wataka uchaguzi bora nchini Kongo

Katika tangazo lao viongozi hao watatu wanasema kwa sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inapitia mojawapo ya nyakati za giza zaidi tangu kuwepo kwake, wakiwataka raia wa Congo kuamka na kuchukua majukumu yao kwa ujasiri na dhamira ili wasiwe mashahidi na washirika wa ukandamizaji wa Congo unaotokana na kutowajibika kwa serikali iliyopo.

Wanadai kuundwa upya kwa tume ya uchaguzi CENI na mahakama ya kikatiba, na pia kusitishwa kwa zana zinazonyima haki wagombea urais.

Fayulu, Matata na Mukwege wanalaumu pia maandalizi ya mchakato wa kuandika wapiga kura wakisema mwanzo wa mchakato huo una hitilafu nyingi.

Akiwa mjini Kinsasa, Dieudonné Mushagalusa ni mwanaharakati wa shirika la raia aliyejaribu kupata kadi ya mchaguzi mbele ya senta kadhaa za kujiandikishia bila kufaulu, na hapa anaeleza.

Chama tawala cha puuza madai ya upinzani

Raia wakosoa ukosefu wa usalama Kivu na Ituri
Raia wakosoa ukosefu wa usalama Kivu na IturiPicha: Augustin Wamenya/AA/picture alliance

Viongozi hao watatu hao Fayulu, Matata na Mukwege wanaonya kwamba fursa hii ya uchaguzi ni muhimu ili kukomesha kabisa migogoro ya mara kwa mara iliojitokeza nchini Congo kuhusu uhalali wa matokeo ya uchaguzi, tangu uchaguzi wa mwaka 2006, kwa hivyo unatakiwa kuandaliwa inavyostahili.

Pia, viongozi hao wanasema inaonekana dhahiri kwamba utawala uliopo, tayari umefanya mfumo wa udanganyifu mkubwa kwa uchaguzi huo.

Upande wa chama tawala cha UDPS,wanachama wanasema huo ni woga tu. Martin Fayulu, Augustin Matata na Denis Mukwege wanadai pia usalama urejeshwe katika eneo la mashariki ya Congo, na pia katika maeneo ya Maindombe na Kwilu ili uchaguzi ufanyike huko katika hali tulivu.

Wanaahidi kuchukua jukumu la kutokubali uchakakuaji wowote ule wa matokeo ya upigaji kura wakati wa uchaguzi wa desemba mwakani na wanasema watahakikisha raia wa Congo wanahamasihwa kuhusu hilo.