1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mzozo wa Mashariki mwa Kongo wazidi kuleta wasiwasi

27 Machi 2024

Watu kumi na mbili waliokimbia vita vya M23 siku kumi zilizopita wamekufa kusini mwa eneo la Lubero na Kanyabayonga. Zaidi ya watu 200,000, wanakabiliwa na njaa kutokana na mgogoro wa hali ya kibinadamu.

https://p.dw.com/p/4eC1k
Mkimbizi wa ndani wa Kongo Claudine akiwa na watoto wake
Mama huyu akiwa amejenga kijumba cha kujihifadhi baada ya kukimbia mapigano huko mashariki ya Kongo. Watu kama hawa wanakabiliwa na madhila makubwa kutokana na ukosefu wa misaadaPicha: Edith Kimani/DW

Kanyabayonga, Lubero katika Kivu ya Kaskazini, na Minova, katika Kivu ya Kusini, ni kati ya maeneo yenye wakimbizi wengi zaidi, lakini, ni miongoni mwa maeneo yanayosahaulika sana linapokuja suala la msaada wa kibinadamu.

Baadhi ya maeneo ya wakimbizi wa vita hayafikiwi na misaada ya kibinadamu katika mikoa ya Kivu Kaskazini na kivu Kusini kutokana na kuzingirwa.

Soma pia:Takriban raia 11 wameuawa mashariki mwa DR Congo

Msaada wa kibinadamu haufiki kwa watu wenye mahitaji na juhudi za kufikisha msaada wa kibinadamu katika maeneo haya yaliyozingirwa zimekwama.

Wafanyakazi wa kibinadamu wanathibitisha kushindwa kwao kufikia baadhi ya maeneo, siyo kwa sababu ya hofu, bali kwa sababu si rahisi kufikia baadhi ya maeneo ambayo yanadhibitiwa na waasi wakati wote.

Msaidizi wa shughuli za kibinadamu ambaye hakutaka kutajwa  jina lake amesema haya alipozungumza na DW "Hali huko Kivu Kaskazini ni ngumu sana kwa sasa. Ni wachache wanaoweza  kufikia maeneo fulani ya wakimbizi, kwa upande mmoja, watu wanashindwa kufika na kwa upande mwingine, sehemu kubwa ya Kivu Kaskazini imevamiwa na waasi, ambayo inamaanisha kwamba hatuwezi kufika mara kwa mara."

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo |  Wakimbizi katika eneo la Minova
Makumi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita wamesimama katika uwanja wa shule ya msingi huko Minova, mkoa wa Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako wamejihifadhi baada ya kukimbia mapigano.Picha: ALEXIS HUGUET/AFP

Wakati huo huo, wakimbizi wa vita walioko katika maeneo yaliyozingirwa zaidi wanakabiliana na mapigano makali. Wakimbizi 12 wamepoteza maisha katika kipindi cha siku 10 tu kutokana na njaa na ukosefu wa huduma za matibabu, kama anavyothibitisha Aimé Mbusa Mukanda, mwanaharakati wa shirika za kiraia

Soma pia:M23 wadhibiti eneo jingine wakati mapigano yakiendelea kwa siku ya tatu Kongo

Zaidi ya wakimbizi 12 wamefariki kwa njaa kutokana na kukosa dawa ndani ya eneo la Kitala na kwenye eneo la Kanyabayonga Rutshuru ambako kuna wakimbizi waliokimbia vita Rutshuru, Kibirizi na Nyanzale. 

"Na wakati nilipozungumza na wakubwa wa makambi, wanakiri kwamba serikali ilituma misaada, lakini haukuwafikia vizuri hawa wakimbizi. Na tunahofia kwamba hao wanasiasa wamefanya ubadhirifu kwenye fedha hizo. Na ndio maana tunaomba serikali iongeze nguvu ili kujua hiye fedha imepotelea wapi hasa na akamatwe," amesema Aimé Mbussa Mukanda wa mashirika ya kiraia.                   

Wakimbizi wa Vita walioko katika maeneo yanayofikiwa na misaada michache ya kibinadamu bado wanakabiliwa na hatari kubwa ya kifo, ambayo inaelekea kwenye janga la kibinadamu, ikiwa serikali haitachukua hatua muhimu na serikali ya Kongo pamoja na Jumuiya ya kimataifa.

Soma pia:Mukwege aonya kuhusu kuondoka haraka jeshi la MONUSCO