1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waomba Wasudan wasisahauliwe

7 Februari 2024

Umoja wa Mataifa leo umeyataka mataifa ya dunia kutowasahau raia walionaswa katika vita vya Sudan na kutoa wito wa dola bilioni 4.1 ili kuyakidhi mahitaji yao ya kiutu.

https://p.dw.com/p/4c8Vl
Wakimbizi wa Sudan nchini Chad.
Wakimbizi wa Sudan nchini Chad.Picha: Marie-Helena Laurent/WFP/AP/picture alliance

Afisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kiutu (OCHA) katika taarifa ya pamoja na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) wamesema fedha hizo pia zitatumika kuwashughulikia wale waliokimbilia mataifa jirani.

Umoja wa Mataifa unasema watu milioni 14.7 wanahitaji misaada huku milioni 1.5 kati yao wakiwa wamekimbilia Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.

Soma zaidi: Watoto 13 wafa kila siku kwa utapiamlo Darfur - MSF

Haya yanajiri wakati ambapo pande zinazozozana nchini Sudan zikiwa zimekubaliana kukutana kwa mazungumzo nchini Uswisi, ili kutoa nafasi ya misaada inayohitajika mno katika nchi hiyo.

Mkuu wa Shirika la Misaada la Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths, amewaambia waandishi wa habari kuwa amezungumza na wakuu wa pande zinazopigana na wote wakakubali kukutana ili kujadili utoaji wa misaada.