1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto 13 wafa kila siku kwa utapiamlo Darfur - MSF

7 Februari 2024

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) linasema watoto 13 hufa kila siku kutokana na utapiamlo katika kambi ya Zamzam iliyoko kaskazini mwa Sudan, yakiwa ni matokeo ya vita vilivyodumu kwa miezi 10 sasa.

https://p.dw.com/p/4c8BF
Sudan, wakimbizi, utapiamlo
Mmoja wa wakimbizi wa ndani nchini Sudan akiwa amembeba mtoto wake.Picha: Marie-Helena Laurent/WFP/AP/picture alliance

Kulingana na Mkuu wa Kitengo cha Msaada wa Dharura cha MSF, Claire Nicolet, mtoto mmoja anakufa kila baada ya masaa mawili kambini humo na wengine wako kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha katika kipindi cha wiki tatu hadi sita ikiwa hawatapata matibabu.

MSF inasema kuwa awali kambi ya Zamzam yenye watu 300,000 ilikuwa ikiwapokea watu wanaokimbia ghasia za kikabila katika eneo la Darfur mwaka 2003, lakini tangu vita vilipozuka kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF mnamo Aprili 2023, wakaazi wa kambi hiyo wamekosa kufikiwa na misaada muhimu ya kibinadamu na huduma za matibabu.

Soma zaidi: UN: Miezi sita ya mapigano nchini Sudan yasababisha vifo vya takriban watu 9,000

MSF imeongeza kuwa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa ya misaada yalihama kaskazini mwa Darfur baada ya vita kuanza na yamekuwa wakihudumia watu kwa kiasi kidogo tangu wakati huo.

Wakimbizi Darfur
Wakimbizi wa Sudan wakigaiwa chakula kwenye kambi iliyopo Chad.Picha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

"Hakuna chakula kinachofika kambini hapa kutoka Shirika la  Mpango wa Chakula Duniani (WFP) tangu mwezi Mei 2023 na watu wanakufa njaa." Alisema Nicolet.

Grandi: Bila misaada na muafaka, wakimbizi wa Sudan watamiminika Ulaya

Wakati huo huo, Mkuu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), Filippo Grandi, alionya kuwa Ulaya huenda ikalazimika kukabiliana na ongezeko la wakimbizi wa Sudan, ikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya pande zinazozozana nchini humo hayatafikiwa na juhudi za kutoa misaada hazitaimarishwa.

"Bila nyongeza ya misaada, wakimbizi kutoka Sudan watajaribu kufanya kutumia njia ili kuingia Ulaya." Alisema Grandi, akiongeza kwamba nchi kadhaa jirani na Sudan kama vile Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini na Ethiopia, "zina udhaifu wao na hazitaweza kuwapa wakimbizi msaada wa kutosha."

Wakimbizi watoto kutoka Darfur wakipata chakula kwenye kambi nchini Chad.
Wakimbizi watoto kutoka Darfur wakipata chakula kwenye kambi nchini Chad.Picha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Soma zaidi: Makabila ya Darfur huenda yakavibadili vita Sudan

Mkuu huyo wa UNHCR alisisitiza kwamba wakimbizi watasonga mbele zaidi kuelekea nchi za kaskazini kama Tunisia, ambako baadhi yao wameripotiwa kupanga kuvuka kuingia Ulaya, na kwamba migogoro katika maeneo kama Sudan, Kongo, Afghanistan na Myanmar haipaswi kupuuzwa wakati wa vita vya Ukraine na Gaza.

Hata hivyo, MSF imesema kwamba itaongeza kwa kasi kiwango cha usaidizi katika kambi ya kutoa matibabu kwa watoto walio katika hali mbaya zaidi lakini, kiwango cha maafa kinahitaji majibu ya haraka.

Zaidi ya watu milioni 9 wanadhaniwa kuwa wakimbizi wa ndani ya Sudan, na wakimbizi milioni 1.5 wamekimbilia nchi jirani katika miezi 10 ya mapigano kati ya jeshi la Sudan likiongozwa na Jenerali Abdel Fattah Burhan dhidi ya kundi la wanamgambo linaloongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo.

Umoja wa Mataifa unasema takribani watu 12,000 wameuawa katika mzozo huo, ingawa vikundi vya madaktari wa ndani vinasema idadi ya kweli inaweza kuwa juu zaidi.