1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tshisekedi apendekeza nafasi rasmi ya msemaji wa upinzani

Jean Noël Ba-Mweze
23 Januari 2024

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi amependekeza upinzani kuanzisha wadhifa wa msemaji rasmi utakaotolewa kwa chama kilichopata kura nyingi katika uchaguzi wa Desemba 20.

https://p.dw.com/p/4baGt
Picha mchanganyiko ya wanasiasa wa DR Kongo Moise Katumbi, Martin Fayulu na Felix Tshisekedi
Wagombea wakuu katika uchaguzi uliyopita, Moise Katumbi (kushoto), Martin Fayulu, (katikati) na Felix Tshisekedi.

Matamshi hayo aliyatoa Jumamosi iliyopita wakati alipoapishwa. Chama ambacho kimepata wingi wa kura ni cha Ensemble Pour la République cha Moïse Katumbi, ingawa hata hivyo bado hakijatoa jibu lolote kuhusu pendekezo hilo, huku muungano wa Lamuka wa Martin Fayulu ukieleza upo tayari kwa majadiliano.

Raïs Tshisekedi alitoa pendekezo hilo katika hotuba wake wa kuapishwa baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Desemba 20 ingawa upinzani bado haujakubali matokeo ya uchaguzi huo ambayo yalitangazwa na tume huru ya uchaguzi na kuthibitishwa na mahakama ya katiba.

Soma pia: Rais wa Kongo aapishwa kwa muhula wa pili mbele ya kadamnasi

Chama cha MDVC cha Justin Mudekereza, mmoja wa wagombea urais ambao hawakufanikiwa, kimeonyesha kuwa na mashaka kuhusu Rais Tshisekedi kutimiza anayoyasema, kwani amejulikana kutoa ahadi zisizotimizwa.

''Kama kwa sasa rais wa jamhuri anasema ukweli na anayo nia ya kulisukuma bunge kutekeleza hayo, wapinzani wanao uwezo wa kukubaliana katika suala hilo.

Kuapishwa kwa Rais Félix Tshisekedi - 20. Januari 2024
Rais Felix Tshisekedi akikagua gwaride siku ya kuapishwa kwake kwa muhula wa pili mjini Kinshasa, Januari 20, 2024.Picha: Paul Lorgerie/DW

Tunachotaka kukiona sisi ni ukweli ila siyo mambo kuainishwa pamoja na ahadi nyingine kadhaa zinazotolewa bila kutimizwa," alisema Augustin Bisimwa, katibu mkuu wa chama cha MDVC.

Lamuka ipo tayari kwa mazungumzo

Upande wake, muungano wa upinzani wa Lamuka umesema upo tayari kwa mazungumzo, lakini bado unaonekana kushughulika na kupinga matokeo ya uchaguzi.

"Martin Fayulu, Moise Katumbi na wengine hawajashindwa. Félix Tshisekedi siye mshindi. Kwa hiyo ni mhimu kuzungumza na kila mmoja ili kuepusha Wakongo kuendelea kudharaulika.

Soma pia: Vyama tawala Kongo vya pata wingi wa viti bungeni

Sisi tupo tayari kujadili ili kutoa majukumu kuhusiana na machafuko katika uchaguzi," alisema Prince Epenge, mmoja wa wasemaji wa kundi la Lamuka.

Wadhifa wa msemaji wa upinzani tayari umepangwa na katiba ya Kongo, lakini haujawahi kutekelezwa tangu uchaguzi wa kwanza hapa nyumbani mwaka 2006.

Chama cha Ensemble Pour la République ambacho kiongozi wake ni Moise Katumbi ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa rais, bado hakijatoa msimamo wake rasmi, huku kikisubiri matokeo ya mkutano wake wa ndani.

Lakini pendekezo la kuunda wadhifa wa msemaji wa upinzani linaweza likawagawanya wapinzani.