1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaza yapigwa mabomu huku UN ikisisitiza upelekwaji msaada

Bruce Amani
25 Machi 2024

Mashambulizi ya angani na ardhini yameendelea kurindima katika maeneo ya Gaza wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akitoa wito wa kuongezwa kwa msaada katika eneo hilo lililozingirwa.

https://p.dw.com/p/4e4v4
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alijionea mwenyewe hali ilivyo katika kivuko cha Rafah cha kuingia GazaPicha: Khaled Desouki/AFP/Getty Images

Viongozi wengine wa ulimwengu wamepaza sauti zao kwa kutoa wito wa kusitishwa mapigano maramoja na kusitishwa kwa mipango ya Israel ya kuwapeleka wanajeshi kupambana na wanangambo katika mji wa kusini mwa Gaza uliofurika wa Rafah.

Mazungumzo yanayolenga kupata muafaka wa kuwekwa chini silaha na kuwachiwa mateka yanaendelea Qatar lakini wakuu wa mashirika ya ujasusi ya Israel na Marekani waliohusika katika mazungumzo hayo wameondoka katika taifa hilo la Ghuba kwa ajili ya mashauriano. Huku Umoja wa Mataifa ukionya kuhusu hatari ya kuzuka baa la njaa huko Gaza, Guterres ameitaka Israel kuruhusu msaada zaidi kuingizwa kupitia kivuko cha Rafah.

Jeshi la Israel limejibu kwenye mitandao ya kijamii likisema kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuimarisha nyenzo zake na kuacha kuilaumu Israel kwa mapungufu yao.