1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Biden na Xi wakubaliana kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano

Bruce Amani
16 Novemba 2023

Rais Joe Biden wa Marekani na Xi Jinping wa China wamekubaliana kurejesha mawasiliano ya kijeshi kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/4Yrlv
Rais Joe Biden wa Marekani na mwenzake wa China, Xi Jinping.
Rais Joe Biden wa Marekani akisalimiana na Xi Jinping wa China walipokutana kwa mazungumzo mjini San Francisco.Picha: THE WHITE HOUSE/UPI Photo/IMAGO

Marais hao walikubaliana katika mkutano wao wa kwanza wa kilele kuandaliwa katika mwaka mmoja.

Biden na Xi walisalimiana kwa mikono kabla ya mazungumzo yao ya saa nne yaliyojikita katika kuzuia mivutano inayoongezeka kati ya madola hayo mawili makubwa duniani kugeuka kuwa mzozo mkubwa.

Pia walikubaliana kuwa China itadhibiti uzalishaji wa dawa za kulevya za opioid ambazo zimekuwa janga nchini Marekani. Rais Xi amesema China iko tayari kushirikiana na Marekani

Hata hivyo Xi na Biden waliendelea kutofautiana kuhusu suala la Taiwan, huku rais wa China akimtaka mwenzake wa Marekani kukoma kukipa kisiwa hicho silaha za kivita na kwamba suala la kuungana tena halizuiliki.

Hata hivyo, Biden baada ya mkutano huo aliwaambia waandishi wa habari kuwa bado anamzingatia Xi kuwa dikteta. Kauli hiyo imelaaniwa vikali na China.