1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

China yasema matamshi ya Biden kumuita Xi dikteta ni upuuzi

Iddi Ssessanga
21 Juni 2023

China imeyataja matamshi ya Rais wa Marekani Joe Biden akimuelezea Rais Xi Jinping kama dikteta kuwa ya kipuuzi na kutowajibika, huku Urusi ikisema matamshi hayo yanaonyesha undumila kuwili wa sera ya kigeni ya Marekani.

https://p.dw.com/p/4Stnj
Joe Biden und  Xi Jinping
Picha: Susan Walsh/AP/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Mao Ninga amesema matamshi ya Biden yanakwenda kinyume kabisaa na ukweli na yanakiuka itifikaki ya kidiplomasia na kuhalifu heshima ya kisiasa ya China.

Akizungumza katika tukio la kuchangisha fedha mjini California Jumanne usiku, Biden alisema Xi alikuwa amefadhaika kuhusiana na mvutano wa karibuni kuhusu puto la China linaloshukiwa kuwa la kijasusi lililodunguliwa na jeshi la anga kwenye pwani ya mashariki.

"Matamshi hayo yamekiuka ukweli wa kimsingi na itifaki ya kidiplomasia na heshima ya kisiasa ya Uchina. Ilikuwa uchochezi wa wazi wa kisiasa. China haijaridhishwa hata kidogo na matamshi hayo na inayapinga vikali," alisema Mao Ning kwenye mkutano wa kila siku na waandishi habari.

Mao amekariri madai ya China kwamba puto hilo lilikusudiwa kufanya utafiti wa hali ya hewa na lililipuliwa kwa bahati mbaya, na kuongeza kuwa Marekani ilipaswa kushughulikia suala hilo kwa njia ya ueledi zaidi.

Indonesien G20 Joe Biden und Xi Jinping
Xi na Biden walipkutana kando ya mkutano wa kilele wa G20 huko Nusa Dua katika kisiwa cha Indonesia cha Bali, Novemba 14, 2022.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Lakini amesema Marekani ilipotosha ukweli na ikatumia nguvu kupiga kelele juu ya tukio hilo, ikionyesha kikamilifu hulka yake ya  uonevu na udhibiti wake wa dunia.

Kremlin yaelezea undumila kuwili wa Marekani

Ikulu ya kremlin imetumia matamshi hayo ya Biden kama nafasi ya kuikosoa Washington, huku ikitilia mkazo uhusiano wake wa karibu na Beijing.

Msemaji wa Kremlina Dmitry Peskov, amewaambia waandishi habari kwamba kuna mkanganyiko kati ya matamshi ya Biden na juhudi za waziri wake wa mambo ya nje, Antony Blinken, kupunguza mzozo na Beijing, wakati wa mkutano na Xi mapema wiki hii.

Soma pia: Matumaini yarejea katika mahusiano ya Marekani na China

"Haya ni maonyesho yanayokinzana sana ya sera ya kigeni ya Marekani, ambayo inazungumzia kipengele kikubwa cha kutotabirika," Peskov aliwaambia waandishi wa habari Jumatano.

"Lakini, hiyo ndiyo biashara yao," Peskov alisema. "Tuna uhusiano wetu mbaya na Marekani na uhusiano wetu mzuri sana na Jamhuri ya Watu wa China.

China | US Außenminister Blinken in China
Rais wa China Xi Jinoing akisalimiana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, mjini Beijing, Juni 19, 2023.Picha: Li Xueren/Xinhua/IMAGO

Ziara ya Blinken ilikuwa imepangwa kufanyika mwezi Februari, lakini ilisitishwa baada ya kudunguliwa kwa puto hilo, na wakati kufanyika kwake wiki hii kumeashiria kurejea kwa mawasiliano ya ngazi ya juu kati ya pande zote, China inaendelea kukataa mazungumzo kati ya majeshi ya mataifa hayo mawili.

Katika siku za karibuni, Marekani inasema ndege na meli za kivita za China zimekwaruzana kwa njia za hatari na za wenzao wa Marekani katika ujia wa bahari wa Taiwan na bahari ya China Kusini, licha ya makubaliano kati yao kuhusu itifaki ya kuepusha matukio kama hayo.

Soma pia: Biden asema mahusiano na China yanafuata "mkondo sahihi"

Wakati wa ziara ya Blinken, China ilikariri upinzani wake dhidi ya msaada wa Marekani kwa kisiwa cha Taiwan chenye kujitawala, ambacho Beijing inadai kuwa sehemu ya eneo lake. Marekani pia imetaka kuizuwia China kupata teknolojia ya uzalishaji wa chip za computer ambayo inaweza kutumia kwa malengo ya kijeshi, na kuituhumu kuiba hati miliki za Marekani.

Chanzo: Mashirika