1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukraine: Urusi inapanga kushambulia mitambo ya nyuklia

Hawa Bihoga
25 Septemba 2024

Mzozo unaoongezeka katika kanda ya Mashariki ya Kati na vita nchini Ukraine vitachukua nafasi muhimu katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo. Rais Zelensky ameiambia hadhira hiyo kwamba urusi imepanga mashambulizi.

https://p.dw.com/p/4l4iM
Marekani | Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Bryan R. Smith/AFP

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya kikao cha dharura kuhusu hali ya nchini Lebanon, huku waandamanaji zaidi ya 30 wanaopinga vita vya Gaza walikamatwa huko Manhattan jana usiku. 

Polisi ilizuwia maandamano hayo kufika Umoja wa Mataifa, lakini pia polisi imesema wanatarajia maandamano zaidi kuendelea.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo majira ya saa 12 kwa saa za Marekani, na mjadala utajikita juu ya Lebanon na ongezeko la mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah.

Lakini muda mchache uliopita, Rais wa Ukraine Volodymryr Zelenskiy amelihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo amesema Urusi inapanga kufanya mashambulizi dhidi ya mitambo ya nyuklia ya Ukraine pamoja na miundombinu, na ameitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za taifa lake kufikia amani.

Soma pia:Ulimwengu wataka Mashariki ya Kati isitumbukie vitani

Zelenskiy alianza hotuba yake kwa kutoa simulizi kuhusu siku za kwanza za uvamizi wa Urusi mnamo mwaka 2022 na utekaji wa kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhia, kabla ya kutangaza kile alichokiita ratiba ya amani, ambayo nukta yake ya kwanza inahusu usalama wa nyuklia.

"Hiki ndiyo chanzo kikuu cha hatari ya miali barani Ulaya, na yumkini kote duniani. Ndiyo maana, katika ratiba ya amani niliyowasilisha, nukta ya kwanza inahusu usalama wa nyuklia."

Aliongeza kuwa "nchini Ukraine tunajua hasa nini tunashughulika nacho, na nataka kuwashukuru wanachama wa Baraza Kuu kwa kuidhinisha azimio la Julai mwaka huu, kuhusu usalama wa vituo vya nyuklia nchini Ukraine."

Rais huyo wa Ukraine amekumbushia kuwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitaka Urusi kurejesha udhibiti wa mtambo wa Zaporizhizhia kwa Ukraine, na kuongeza kuwa ni hapo tu ndiyo usalama wa kweli wa nyuklia utarejea barani Ulaya na kote duniani.

Mpango wa amani wa Ukraine

Zelenskiy pia amehoji maslahi ya kweli ya China na Brazil kushinikiza amani nchini Ukraine, na kusema mataifa hayo hayawezi kuimarisha nguvu yake kwa gharama ya Ukraine.

Hotuba ya Zelenskiy ilifuatiwa na ile ya Rais wa Ghana Nana Akufo Ado, ambaye pia amekosoa kushindwa kwa chombo hicho cha ulimwengu kuzuwia uvamizi wa Urusi dhidi ya jirani yake. 

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

Rais Nana Akufo Ado amezungumzia pia mapinduzi ya kijeshi yaliyozikumba nchi kadhaa za Afrika Magharibi na kusema hali hiyo inarejesha nyuma demokrasia, huku akiahidi kuwa uchaguzi wa mwaka huu nchini mwake utakuwa huru na wa haki.

Hapo Jumanne, Rais Zelenskiy aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwamba Urusi inapaswa kulaazimishwa kurudisha amani. Urusi imekosoa vikali hatua hiyo ya Zelenskiy kuzungumza mbele ya Baraza la Usalama.

Msemaji wa ikulu ya Urusi D'mitry Peskov, amesema nchi kulazimishwa kufikia amani ni kosa kubwa sana.

Soma pia:Hotuba za viongozi UNGA kuuanza kutolewa rasmi Jumanne

Wakati huo, huo, Rais wa Marekani Joe Biden ameandaa hafla ya viongozi wa dunia ili kuzindua tangazo la pamoja la kuunga mkono ufufuaji wa Ukraine na ujenzi mpya. 

Hata hivyo mwaliko wa waziri mkuu wa Georgia, Irakli Kobakhidze, kwenye hafla hiyo umeondolewa, kulingana na vyombo vya habari vya nchi hiyo, katika pigo kwa uhusiano uliowahi kuwa wa karibu kati ya Georgia na Marekani.

Maafisa wa Georgia wameviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa Kobakhidze. ambaye amepangiwa kuhutubia UNGA kesho Alhamisi, alikuwa amealikwa awali kwenye hafla hiyo, lakini mwaliko wake ulifutwa na upande wa Marekani, na kwamba Marekani ilikataa mikutano yote na ujumbe wa Kobakhidze.