1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroBurkina Faso

Zaidi ya watu 10 wameuawa katika shambulio Burkina Faso

26 Agosti 2024

Watu kadhaa, wakiwemo raia wameuawa katika shambulio lililofanywa na watu waliokuwa na silaha katika kijiji cha Barsalogho nchini Burkina Faso.

https://p.dw.com/p/4ju08
Burkina Faso | Armee Putschisten Traore
Jeshi la Burkina Faso likishika doria OuagadougouPicha: Kilaye Bationo/AP/dpa/picture alliance

Hayo yameelezwa na vyanzo vya usalama jana Jumapili.

Mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kuwa, makundi ya watu waliokuwa na silaha walishambulia kijiji na kuua raia na maafisa wa usalama mwendo wa saa tatu asubuhi jana.

Afisa wa usalama ambaye hakutaka jina litajwe amesema zaidi ya watu kumi wameuawa, wakiwemo raia na vikosi vya usalama pamoja na majeruhi wengi.

Soma pia: Burkina Faso yamulikwa kuhusu utekaji nyara wanaharakati na waandishi

Majeruhi hao wamepelekwa katika hospitali iliyoko katika mji mkuu wa mkoa wa Kaya, umbali wa kilomita 45 kutoka eneo la tukio.

Kulingana na chanzo cha hospitali, zaidi ya watu 100 wamefikishwa hospitalini humo.

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na shambulio hilo.

Makundi ya watu wenye silaha walio na mafungamano na kundi la kigaidi la Al-Qaeda na lile linalojiita Dola la Kiislamu IS, yamekuwa yakiendesha uasi nchini Burkina Faso tangu mwaka 2015 na kuwaua maelfu ya watu na kusababisha watu milioni mbili kuyahama makaazi yao.