1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

WHO: Chanjo za mpox kuwasili hivi karibuni DRC

31 Agosti 2024

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa shehena ya kwanza ya chanjo ya virusi vya homa ya nyani (mpox ) inatarajiwa kuwasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika siku zijazo.

https://p.dw.com/p/4k7mh
DR Kongo | Rais Felix Tshisekedi  na Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus (kushoto) akisalimiana na rais wa DRC Felix TshisekediPicha: DRC Presidency/Xinhua News Agency/picture alliance

Hayo yameelezwa na mkuu wa  WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus baada ya kurejea siku ya Ijumaa kutoka nchini Kongo huku akisema kuwa katika siku zijazo chanjo zaidi zitawasilishwa nchini humo.

Agosti 14 mwaka huu, WHO ilitangaza hali ya dharura ya kimataifa kutokana na kusambaa kwa virusi vya mpox, hasa kuongezeka kwa visa vya maambukizi vya aina mpya ya virusi hivyo inayofahamika kama Clade 1b nchini Kongo na katika nchi jirani.

Soma pia: Papa Francis atoa mwito wa msaada zaidi kwa wagonjwa wa mpox

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani - WHO, karibu visa 15,000 vya mpox vimegundulika nchini Kongo katika mwaka wa 2024, huku kukiwa na vifo 500.

Mataifa mbalimbali yaahidi kuisaidia DRC kupambana na Mpox

DRCongo | Mgonjwa wa Mpox
Mgonjwa wa Mpox nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya KongoPicha: Ruth Alonga/DW

Serikali ya Ujerumani imesema itapeleka Kongo maabara ya kuhamishika ili kusaidia kuwagundua wagonjwa wa homa ya Mpox na kudhibiti kuenea kwa maambukizi.

Soma pia: Ufadhili wa mapambano ya Mpox Afrika wachechemea

Wizara ya Ushirikiano wa Kimaendeleo wa nchi hiyo imesema pia kuna mipango ya kutoa mafunzo kwa wataalamu zaidi ili waweze kutambua dalili na kuufahamisha umma kuhusu hatua za kuzuia ugonjwa huo.

Kwa upande mwingine, Serikali ya Uingereza iliiahidi siku ya Jumatano Kongo kitita cha pauni milioni 3.1 kwa ajili ya kusaidia kupambana na mripuko wa  homa ya Mpox ambao tayari umeshauwa watu zaidi ya 500 na kuathiri wengine kadhaa.

(Vyanzo: AP, DPAE, AFP)