1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliopona Ukimwi, matumaini ya vita dhidi ya ugonjwa huo

25 Julai 2024

Watu watatu waliopona kabisa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wamezungumzia namna tiba hatari ya upandikizaji wa uloto ilivyookoa maisha yao.

https://p.dw.com/p/4ijhY
Deutschland München 2024 | Eingang zur Welt-Aids-Konferenz vor Eröffnung durch Bundeskanzler Scholz
Picha: Sabine Dobel/dpa/picture alliance

Wameyasema haya huku mmoja akidai ni uthibitisho unaoishi juu ya matumaini ya mapambano dhidi ya virusi hivyo.

Watu hao walizungumzia tiba hiyo kwenye mkutano wa kimataifa wa UKIMWI mjini Munich, Ujerumani, uliowakutanisha wataalamu, watafiti na wanaharakati kujadili hatua zilizofikiwa katika kupambana na janga hilo.

Sharon Lewin, Rais wa Jumuiya ya Kimataifa ya masuala ya UKIMWI amesema shuhuda hizi zinatoa mwanga wa mwelekeo wa kupatikana kwa tiba ya VVU.

Matukio haya tunayoyazungumzia leo yanasisimua sana. Yanatia moyo. Yanatupa mawazo mapya ya kujaribu, lakini ni matukio ya nadra sana. Ni watu saba tu kati ya watu milioni 40 wanaoishi na VVU waliopata tiba hiyo. Kwa hivyo ni matukio ambayo ni ya nadra sana, lakini yanahamasisha mwelekeo mpya katika sayansi," alisema Lewin. 

Watu hao saba wanaaminika kupona kabisa baada ya kupandikizwa uloto, tiba yenye maumivu makali na hatari inayotolewa kwa watu wenye virusi hivyo pamoja na saratani mbaya ya damu.