1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita dhidi ya umaskini nchini Niger

ELIZABETH KEMUNTO4 Agosti 2004

Mwaka wa 1980 ulikuwa mwaka wa mabadiliko nchini Niger. Soko la madini ya uranium lilianguka ghafla duniani na tangu hapo nchi hiyo imekumbwa na matatizo ya kiuchumi. Hali imekuwa mbaya zaidi kufuatana na ukame ambao umesababisha umaskini katika sehemu za mashambani na mijini.

https://p.dw.com/p/CHie

Wakazi wa mji mdogo wa Koira Tegui ulioko karibu na mji mkuu Niamey, wanaishi katika hali ngumu za kiuchumi bila msaada wowote. Adds Daouda Ali ni kiongozi wa kijamii katika mji huo na anasema hakuna barabara katika sehemu hiyo na kituo cha afya ni kimoja tu.Kisima cha kuteka maji ni kimoja na hakitimizi mahitaji ya kila moja.

Amadou Ibrahim ni mtaalam wa kiuchumi katika afisi ya benki ya dunia mjini Niamey, na anasema kuwa viongozi wa Niger wameona haja ya kuufanya uchumi wa nchi hiyo kuacha kutegemea madini ya urenium. Hata hivyo wazo hili halijawahi kuchukuliwa hatua yoyote.

Katika hotuba za viongozi hawa, wanasisitiza kwamba ukulima na mifugo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Niger. Jambo la kushangaza hata hivyo ni kuwa hakuna sera za kiuchumi zinazoonyesha jinsi sekta hizi mbili zitafaidi nchi hiyo. Kwa mfano hakuna yule ambaye amejaribu kuanzisha viwanda vya pamba au njugu au hata miradi katika sekta ya kibinafsi.

Kulingana na ripoti ya Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa UNDP, asilimia 63 ya watu nchini Niger wanaishi chini ya kiwango cha chini kabisa cha umaskini. Kukosa chakula cha kutosha na nyumba nzuri ni tatizo kubwa.

Katika jitihada za kukabiliana na tatizo hili serikali ikishirikiana na wadhamini ilichukua mkakati wa kupunguza umaskini mnamo Januari 2002. Mpango huu unalenga kuendeleza ukulima na sekta zingine na kuhakikisha kuwa huduma za kijamii zinatolewa kwa wananchi.

Mbali na hayo mkakati huo unajumuisha hatua ya rais ya kujenga madarasa elfu moja, zahanati elfu moja na mabwawa kadhaa. Hatua hii pia inahusika na kuongeza nafasi za kazi.

Mpango huu ulianzishwa mwanzoni mwa 2001 na unapata fedha kutoka kwa shirika linalotoa misaada kwa nchi zenye madeni makubwa. Lengo la mpango huu ni kuboresha mapato ya sehemu za mashambani na kuongeza vituo vya afya pamoja na kuongeza idadi ya watoto wanaojiunga na shule za msingi.

Shirika hili la kutoa misaada kwa nchi zenye madeni makubwa, lilianzishwa na Benki ya dunia katika jitihada za kuzipa nafasi nchi maskini, kupunguza madeni yao ya kigeni na kutimiza miradi ya kupunguza umaskini.

Kupitia mpango huu, idadi ya kujiandikisha katika shule za msingi ilipanda kutoka asilimia 37 mwaka wa 2000 hadi asilimia 47 mwaka wa 2002. Mbali na hayo mpango huo ulihusika katika kuongezeka kwa nafasi za kazi . Kazi hizi mpya zilikuwa katika sekta za kilimo, elimu na uvuvi. Huduma za afya pia zimekuwa bora zaidi.

Licha ya jitihada hizi za serikali za kupunguza umaskini sio kila mtu amefurahishwa. Adamou Abdou ni msimamizi wa shirika lisilo la kiserikali la kusaidia wanawake kutoka sehemu za mashambani. Adamou analalamika kuwa jamii zinazohusika na miradi hii hazijahusishwa na jinsi miradi hii imefanywa. Kwa mfano utapata kuwa mahala pa kuteka maji pamejengwa mahala ambapo ujenzi wa shule ni muhimu zaidi.

Malamiko hayahaya yanatolewa na mkazi mmoja wa wilaya ya Ouallam ambaye anasema "Kuna haja gani kujenga zahanati au shule na hakuna kinachotendeka katika majengo hayo. Hakuna huduma zinazoendelea."

Hata maafisa wa serikali wanakubali kuwa baadhi ya miradi haikufikiriwa na kupangwa inavyotakikana kabla ya kutekelezwa. Ili kuanzisha huduma katika majengo hayo yaliyoachwa, serikali sasa imeanza kutoa fedha na wafanyakazi wa kutoa huduma hizo.

Matatizo haya yameletea baadhi ya watu wengine kusema kuwa jitihada za serikali za kumaliza umaskini ni njia moja ya kujipatia sifa tu. Fedha zinazotumika katika miradi hii ni dola milioni themanini na moja kwa miaka mitatu lakini kulingana na kiwango cha umaskini nchini Niger, fedha zinazohitajika ni mabilioni kwa kila mwaka ili kupunguza umaskini kwa nusu. Hata hivyo wadhamini kwa upande wao wanafurahishwa na vita dhidi ya umaskini nchini Niger.